2015-04-05 09:13:00

Kongamano la Watawa Kimataifa: Changamoto katika ulimwengu wa digitali


Askofu mkuu Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kama sehemu ya maandalizi ya kongamano la kimataifa kwa ajili ya majiundo awali na endelevu kwa ajili ya watawa wa leo na kesho anabainisha kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anawaandaa watawa watakaokuwa tayari kupambana na changamoato za ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia; watu ambao wanaweza kusimama kidete kutafuta, kulinda na kutetea  misingi ya haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

 

Kongamano hili linaanza kutimua vumbi kwa mkesha hapo tarehe 7 hadi tarehe 11 Aprili 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kufundwa maisha ya kitawa kama kiini cha Kanisa na Ulimwengu”. Mama Kanisa anatambua kwamba, ustawi na maendeleo ya maisha ya kitawa na kazi za kitume sehemu mbali mbali za dunia kwa kiasi kikubwa yanategemea majiundo makini ya awali na endelevu, kwa kuzingatia uaminifu unaojikita katika kipaji cha ugunduzi na usomaji wa alama za nyakati kwa karama za mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

 

Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya mashirika ya kitawa na kazi za kitume kuwa na walezi waliofundwa wakafundika, ili kusaidia mchakato wa majiundo ya watawa wa leo na kesho. Kongamano la malezi ya kitawa kimataifa ni fursa ya kuweza kupembua changamoto, fursa na matatizo yaliyoyopo, ili kuibua mbinu mkakati utakaoyasaidia mashirika ya kitawa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara.

 

Malezi ya kitawa yanasimamiwa kimsingi na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Elimu Katoliki, kwani mabaraza yote haya yanajikita katika majiundo katika medani mbali mbali za maisha ya mtawa, ndiyo maana wakuu wa Mabaraza haya wanashiriki pia katika kongamano hili la malezi kimataifa. Lengo ni kumwandaa mtawa katika medani mbali mbali za maisha.

 

Askofu mkuu Carballo anabainisha kwamba, kati ya changamoto kubwa kwa maisha ya kitawa na kazi za kitume kwa nyakati hizi ni maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, athari zake ni kubwa katika maisha ya watawa wengi. Matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii ni jambo linalopaswa kupewa uzito wa pekee kwani hata matumizi ya mitandao yanasaidia kupata majibu ya mkato, lakini watawa wanapaswa kutambua madhara yake kwa siku za baadaye.

 

Changamoto nyingine ni rasilimali muda inayopaswa kutumiwa vyema, kwa ajili ya sala, kazi, masomo, utume, mazungumzo, maisha ya kijumuiya na kidugu na mapumziko binafsi na yale ya kijumuiya. Rasilimali muda inahitaji nguvu nyingi na uwepo makini wa mtu: kiakili, kiroho na kimwili. Watawa wanapaswa kuwa makini katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, hapa busara na uwajibikaji ni mambo msingi kabisa. Kwani kuwakataza watu kutumia mitandao ya kijamii ni kupitwa na wakati, matumizi yasiyokuwa na busara yanahatarisha maisha na ustawi wa mtawa mwenyewe.

 

Changamoto nyingine inayopaswa kupewa msukumo wa pekee ni ushuhuda wa maisha unaojikita katika mashauri ya Kiinjili, yaani: ufukara, utii na useja kwa kutambua kwamba, walimwengu mamboleo wanainjilishwa kwa haraka zaidi kwa njia ya mifano yenye mvuto na mashiko; watu ambao wanaweza kusikiliza kwa makini na kuwasaidia watu katika shida na mahangaiko yao.

 

Watawa hawana budi kufundwa kikamilifu katika masuala ya haki, amani na upatanisho na kutambua kwamba, wao pia wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu kuiendeleza kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi Tunu hizi msingi katika maisha ya Kikristo zinapaswa pia kumwilishwa katika uhalisia na ushuhuda wa maisha kwa kutambua kwamba, haki inakwenda daima na msamaha. Watawa wawe ni wahudumu bora wa kazi ya uumbaji na kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kuwa ni vyombo vinavyosaidia kutunza mazingira na wala si vinginevyo.

 

Kwa vile watawa wanaishi na kutenda kati ya watu, wanapaswa pia kufundwa kikamilifu katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kwani watawa wanatoka katika misingi ya uhalisia wa maisha ya watu. Hapa watawa wanapaswa kuhibiri kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuendelea kutekeleza changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa. Bado Kanisa linapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa majiundo makini ya watawa katika majadiliano ya kidini na kiekumene.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.