2015-04-05 13:50:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Wajibu wa kijamii wa Kanisa


Zingatieni haki na kutenda mema ndiyo kauli iliyoongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima cha mwaka 2015. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican imekwisha kushirikisha utangulizi, Sura ya kwanza kuhusu haki: Sura ya pili kuhusu ukuu wa haki na tunu zake; sura ya tatu: matukio ya Kikanisa na leo tunakuletea:

SURA YA NNE: WAJIBU WA KIJAMII WA KANISA

17. “Wito wa binadamu ni kudhihirisha sura ya Mungu”. Kanisa linazingatia wazo hili katika roho ya utume wake. Ni kwa sababu hii, Kanisa haliwezi kufumbia macho wajibu wake katika kuchangia makuzi ya jamii na kuhimiza “unyofu wa mwenendo”.9 Himizo la kuzingatia haki na kutenda mema, ni himizo linalolitaka Kanisa lijihusishe na jamii. “Mimi ni mwanadamu, hakuna suala linalomuhusu mwanadamu yeyote ambalo halinihusu”. Kila mara Kanisa linapotimiza wajibu huu linashutumiwa kuingilia siasa. Tafsiri hiyo ni potofu. Swali la kujiuliza ni hili kwamba, “siasa ni nini?”. Kama siasa ni mfumo wa maisha unaowahusu watu, Kanisa haliwezi kukaa pembeni. Kanisa likikaa pembeni litatenda dhambi ya kutotimiza wajibu kwa jamii. Kwani, “furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na wale wote wanaoteswa yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasiwa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao”. Ni vema tuzidi kuwakumbusha wanakanisa kuwa wajibu wa kutetea nakulinda haki ni sehemu ya uinjilishaji na umisionari wa Kanisa. Hivyo basi, tusiruhusu kupokonywa furaha ya uinjilishaji na ari ya umisionari huu.

 

18. Dhana ya kudai kwamba Kanisa linaingilia siasa palelinapokosoa mifumo mibovu ya jamii ni upotoshajiwa makusudi. Hata hivyo, Kanisa Katoliki lingependa kutamka wazi kuwa wakati waamini wake wana vyama vyao vya siasa, Kanisa Katoliki halina wala halifungamanina chama chochote cha siasa. Kanisa linafungamana nabinadamu katika hali zake zote, njema na ngumu na lina wajibu wa kinabii wa kuwa “sauti ya wasiokuwa na sauti”. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuliasa Kanisa akisema: “Hutokea wakati mwingine kwambawahanga wa umasikini na kusetwa waamuapo kuanza kutenda kama watu wenye akili timamu na utashi na kudhubutu kukabiliana na vikwazo vya umasikini na manyanyaso, wawakilishi wa Kanisa hujiengua na kujifanya waangalizi tu. Kanisa sharti likubali kwamba maendeleo ya watu humaanisha maasi dhidi ya udhalimu. Iwapo Kanisa halitashiriki kwa vitendo katika maasi dhidi ya mifumo dhalimu ya kiuchumi inayosababisha watu kutoswa katika fedheha ya umaskini na kudhalilishwa, Kanisa halitakuwa na maana yoyote kwa watu na dini ya kikristo itapoteza mvuto na kuwa kamaushirikina ikikubaliwa kwa uoga tu. Iwapo Kanisa, waamini wake na asasi zake, halitadhihirisha upendo wa Mungu kwa watu kwa kushirikiana na watu na kwa kuwaongoza katika kupinga kiungwana maovu wanayotendewa na wadhalimu, basi litahusishwa na utesaji wa watu wote na kutokuwa na  haki kwao. Jambo hili likitokea, Kanisa litakufa, na kwa kufikiri  kibinadamu linastahili kufa”.

 

19. Safari ya Taifa letu katika wakati wetu sasa ni safari inayopitia katika mkanganyiko mkubwa wa kutokujitambua na inayokosa utashi wa dhati wa kuijenga jamii inayokua katika misingi ya haki. Hii ni kwa sababu zipo dalili lukuki za kukosekana kwa uadilifu na  dhamiri safi. “Hadhi ya binadamu yadokeza na kudai  unyofu wa dhamiri adilifu. Dhamiri adilifu ni pamoja na kutambua misingi ya uadilifu”.14 Na kimsingi, “kadiridhamiri inavyozidi kuwa nyofu, ndivyo watu na vikundivinavyozidi kujitenga na uamuzi kipofu na kujaribu (kuishi) kulingana na sheria halisi za uadilifu”.

 

20. Kuinjilisha ni kuufanya uwepo wa Mungu ujidhihirishekatika ulimwengu wetu. Mungu, katika Kristo hamkomboi mtu mmoja mmoja tu, bali pia mahusiano ya kijamii baina ya watu. Ndio maana, katika moyo wa Injili tunaona uhusiano wa kina kati ya uinjilishaji na maendeleo ya mwanadamu.Tusiruhusu kupokonywa furaha ya uinjilishaji na umisionari huu.

 

Mchakato wa Katiba mpya

 

21. Taifa letu linapita katika kipindi cha mchakato wa Katiba mpya. Tunarudia kusisitiza kuwa hiki ni kipindi adhimu kwa Taifa letu. Tunapenda kulikumbusha Taifa letu kwamba hili ni zoezi linalodai uadilifu mkubwa na utashi wa kisiasa wenye lengo la kujenga Taifa kwa muda mrefu. Kejeli, vitisho, migomo, vijembe na kukosa ustahimilivu katika mijadala yenye kulengakuunda misingi ya mustakabali mwema wa Taifa letu vinaonesha kukosekana kwa uzalendo na ukomavu wa kisiasa. Mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania usiwe chimbuko na chanzo  cha kubomoa mema mengi yaliyokwisha kufikiwa kwa  amani, uhuru, udugu na haki.

 

Ikumbukwe kwamba  Katiba ni Mwongozo Mkuu na kiunganishi cha msingi chajamii yetu ya Tanzania. Katiba mpya inapaswa kutujenga katika utamaduni na maisha mapya yatakayotokana na mila na desturi za makabila zaidi ya 130 kwa kujengamisingi mipya iliyosheheni dira mpya, miiko ya uongozi, haki, wajibu na uwajibikaji chini yake au kwa mujibu washeria, kanuni, mila, desturi na mapokeo ya jamii. Kwa nguvu ya katiba bora sisi sote Watanzania wa Bara na  Visiwani tutaweza kuheshimiana kiadilifu, siyo kinafiki;  na jumuiya ya kisiasa na wengine wote walio na mamlaka na nyadhifa za kiutawala na kiuongozi kuwajibika kidemokrasi.

 

Uchaguzi mkuu 2015

 

22. Mwaka huu wa 2015 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuunchini Tanzania. Tutakuwa tunakabiliwa na uamuzi wa kisiasa kwa kuchagua viongozi watakaotumia rasilimaliza taifa letu kwa ama ustawi na maendeleo ya wengiwalio katika lindi la umaskini au kwa matumizi ya faharizao binafsi na wabia wao katika kujitajirisha. Tunashauri zoezi hili liendeshwe kwa uadilifu na lisifanywe kuwatendo la ulanguzi wa kura. Huku ni kudhalilisha utu wawatu na kuvuna madaraka kupitia umasikini wa watu.Tunapenda wale wanaoomba dhamana ya uongoziwa Taifa hili katika nyanja zote na sisi sote tunaotumia haki ya kura zetu tuitumie fursa hii kama dhamana na tendo la heshima ya utu wetu. Matukio haya ya makuzi  ya jamii yetu yasidhoofishe amani yetu. Katika yote  tunawahimiza; zingatieni haki na kutenda mema, mkitenda   yote kwa moyo huru unaoongozwa na dhamiri safi.

 

Hitimisho

23. Wapendwa Taifa la Mungu, sisi Maaskofu wenu tunawatakieni kila baraka katika safari hii ya imani.Tumwombe Mungu aithibitishe Imani yetu nayoijidhihirishe katika maisha na matendo yetu ya kila siku katika kuzingatia haki na kutenda mema.

Ni sisi Maaskofu wenu.

 

BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA.








All the contents on this site are copyrighted ©.