2015-04-04 07:51:00

WCC: Kifo hakina nguvu tena, Yesu ni mshindi!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, linaungana na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa kulaani vikali mauaji ya kinyama yaliyofanyika kwenye Chuo kikuu cha Garissa, Kenya na kusababisha vifo vya wanafunzi 147 na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa vibaya kutokana na shambuli la kigaidi lililofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab. Dr.  Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasikitishwa sana na mauaji haya ambayo yamefanywa kwa misingi ya kidini.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaiomba Serikali ya Kenya pamoja na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanasaidia mchakato wa kuwakamata na kufikisha mbele ya sheria wahusika wote wa vitendo vya kigaidi sanjari na kuweka mikakati zaidi ya ulinzi na usalama kwa siku za usoni. Mashambulizi na mauaji ya kinyama kwa misingi ya kidini ni jambo ambalo ni hatari sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafungamano ya kijamii.

Watu wajitahidi kushinda kishawishi cha chuki na uhasama wa kidini na badala yake wazame zaidi katika majadiliano ya kidini yanayojikita katika misingi ya ukweli, uwazi, upendo na mshikamano wa dhati. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuungana na ndugu, jamaa na marafiki waliowapoteza ndugu zao kutokana na shambulizi hili la kigaidi. Baraza linawaombea majeruhi waweze kupona haraka na kuendelea na masomo yao na kwamba, upendo na mshikamano wa kidugu viendelee kutawala miongoni mwa wananchi wa Kenya.

Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema kwamba, Ujumbe wa Pasaka ni huu: Kifo na mauti havina nguvu tena, Kristo ameshinda yote haya! Ijumaa kuu Makanisa sehemu mbali mbali za dunia yamewakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia, ili wapate faraja kutoka katika Fumbo la Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemtumia Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, salam za rambi rambi kutokana na mauaji ya wanafunzi 147 na kuwataka wananchi wa Kenya kusimama kidete bila woga kupinga vitendo vyote vya kinyama kwa kujikita katika mapambazuko mapya ya mahusiano ya kidugu, haki na amani. Wakati wa Ibada ya Liturujia ya Neno kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa jioni, Padre Raniero Cantalamessa wakati wa mahubiri mbele ya Baba Mtakatifu Francisko, amewakumbuka wanafunzi 147 waliouwawa kikatiliki huko Garissa nchini Kenya. Amesikitishwa sana na ukimya ulioneshwa na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataita kwa kushindwa kukemea vitendo hivi vya kinyama kwa kukaa kimya, kana kwamba, hakuna jambo lolote lililotendeka!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.