2015-04-04 08:43:00

Ujumbe wa Pasaka: fungueni macho na masikio kutetea haki na amani


Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa mwaka 2015, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanafungua macho na masikio yao, tayari  kusimama kidete kutetea haki na amani. Ujumbe wa Maaskofu wa Argentina unaongozwa na kauli mbiu “ Tazama mikono na miguu yangu ni mimi mwenyewe”.

Hii ni changamoto kwa wakristo kuishi kweli za kiinjili kwa kutambua kwamba, wanazungukwa na malimwengu, wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wanatumbukizwa katika matope ya dunia na huko watalia na kusaga meno. Ukweli wa mambo unadhihirisha kwamba, wamezungukwa na vita, ubinafsi, hali ya kutojali na hali ya kubaguana.

Haya ni mambo ambayo yanawakabili waamini katika hija ya  maisha yao ya kila siku, changamoto ni kusimama kidete kwa ajili ya kutetea, kudumisha na kuendeleza mafao ya wengi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutafuta furaha ya wengi, ili kujenga dunia iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Wakristo hawawezi kuridhika kwa kujifungia katika undani wao, bali wanatumwa kutoka nje kuangalia shida na magumu ya jirani zao, tayari kutafuta suluhu ya pamoja, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Machimbo ya madini yanayofanywa na makampuni makubwa ni tishio kubwa kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wengi nchini Argentina. Kwani shughuli hizi za kiuchumi licha ya kuendelea kuyanufaisha Makampuni makubwa ya madini, zimekuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na athari zake zinaonekana kwa maisha ya wananchi wengi wa Argentina.

Maaskofu wanabainisha kwamba, elimu inayotolewa shuleni haina budi kusaidia kujenga utamaduni wa kulinda uhai, mafao ya wengi, maridhiano na mshikamano wa kijamii. Amani ya kweli inaweza kupatikana ikiwa kama kila mwananchi atajitahidi kutekeleza wajibu wake msingi; ikiwa kama watu watakuwa na fursa za ajira na kulipwa ujira unaokidhi mahitaji msingi ya binadamu na kwamba, mapendekezo, maamuzi na utekeleza wa sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo na ustawi wa wengi hayana budi kuwashirikisha wahusika na wala yasiwe ni maamuzi ya watu wachache ndani ya jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunga kibwebwe ili kujenga jamii inayojikita katika upendo na udugu, changamoto kubwa na endelevu na kwamba, mambo ambayo yanatishia amani, ustawi na maendeleo ya wengi yanapata chimbuko lake kutoka katika moyo wa mwanadamu, ambao umeathirika kutokana na dhambi ya asili. Ili kujenga uchumi unaojali na jamii inayowajibika, kuna haja ya jamii kujikita katika Injili ya Uhai,  haki msingi na kukataa katu katu kumezwa na utamaduni wa kifo, chachu ya ubinafsi na uchoyo.

Wananchi wajikite katika utawala wa sheria na kukataa kishawishi cha njia za mkato katika maisha kama vile biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya sanjari na biashara haramu ya binadamu. Kanisa litaendelea kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwajengeaa vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.