2015-04-04 08:17:00

TEC: Watanzania onesheni ukomavu katika: Katiba na Uchaguzi mkuu 2015


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ametoa salamu za Pasaka kwa mwaka 2015 kwa waamini na wote wenye mapenzi mema, na kubainisha kuwa masuala ya uchaguzi mkuu na mchakato wa kupata katiba mpya yanapaswa kudhihirisha ukomavu katika utawala wa kidemokrasia nchini Tanzania.

Askofu Ngalalekumtwa ameelezea umuhimu wa watanzania kudumu katika sala ili taifa linapoingia katika uchaguzi mkuu lilindwe na  Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mfalme wa mataifa yote. “Mwaka huu nchi yetu inashuhudia mambo mawili ambayo yanabeba sura ya Taifa, nayo ni uchaguzi mkuu na mchakato wa kupata katiba mpya. Kwa jinsi hali ilivyo tete tudumu katika sala ili  Mungu aliye mtawala wa mataifa atawale mioyo ya raia na viongozi wa nchi ili shughuli hizo zilindwe kwa mapenzi yake” amebainisha.

Pia amewataka watanzania kuonesha ukomavu na kujua maana ya kujitawala hasa kwa kufuata utawala bora unaozingatia sheria na maadili na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na nyingine ulimwenguni. Ametoa hamasa kwa kila mtanzania kutumika kama chombo cha upendo, haki, amani na umoja katika kutoa huduma kwa watu mbalimbali na taifa kwa ujumla.

Pasaka huashiria mabadiliko chanya

Aidha Askofu Ngalalekumtwa ameeleza kuwa Pasaka ni mwaliko wa kujitakasa ili kuishi maisha ya neema badala ya kuendelea kukumbatia dhambi. Amewataka waamini kuacha mambo ya ovyo ili waweze kushiriki kikamilifu katika ufufuko wa Kristo kwa kuifia dhambi, kwani Pasaka ni kipindi cha kupita, kugeuka, kubadilika na kuzaliwa upya. “Kwa utii, unyenyekevu na uvumilivu wa Yesu Kristo, Mungu alimpatia zawadi kwa kumwambia maneno kuwa ‘Wewe ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa’. Kuzaa kunakozungumziwa hapa ni kurudi katika utukufu wa Mungu Baba. Nasi tunaalikwa kuachana na dhambi ili siku moja Mungu aseme nasi kuwa ‘tu wanawe leo ametuzaa;” amesema Askofu Ngalalekumtwa.

Akielezea juu ya shangwe zinatotawa katika kipindi cha Pasaka, Askofu Ngalalekumtwa amebainisha kuwa ni kipindi cha kumshangilia na kumuinua Mwenyezi Mungu kwa huruma yake kwa wanadamu, pale mwanaye Yesu Kristo alipojitoa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu, kwa uvumilivu na upendo mkubwa kwa kuteswa, kufa hata kufufuka kwake. “Kristo ni ishara ya uwezo mkubwa wa Mungu dhidi ya dhambi na mauti. Anapowatokea wanafunzi wake waliokuwa katika chumba cha karamu ya mwisho anawaambia ‘amani iwe kwenu’, hatoi lawama kuwa ‘kwa nini mliniacha peke yangu’.

Ikiwa Kristo ambaye hakuwa na dhambi alipambana na mahangaiko yote ya maisha hata kusingiziwa, kuteswa na kufa, sisi wenye dhambi yatupasa kuvishinda vishawishi vya dhambi daima” ameongeza. Pia ameeleza kuwa Pasaka ya kweli inajidhihirisha pale Wakristo wanapotembea katika maisha na mwanga wa Kristo Mfufuka, kwa kukumbatia Injili ya Uhai na kukataa katu katu kumezwa na malimwengu.

Na Pascal Mwanache,

Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.