2015-04-04 10:26:00

Papa awataka wananchi wa Colombia kujenga misingi ya haki na amani


Familia ya Mungu nchini Colombia haina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani kama njia muafaka ya ujenzi wa jamii inayojikita katika haki na udugu. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. 

Ujumbe huu umetolewa wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo makuu ya Kanisa, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, anatarajia kukutana na kuzungumza na Familia ya Mungu nchini Colombia wakati wa hija yake ya kitume ambayo bado inaendelea kuandaliwa na viongozi husika.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu Katoliki nchini Colombia kwa kuonesha mshikamano na upendo wa kidugu katika utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa hususan katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Anatambua changamoto kubwa zilizoko mbele yao wakati huu wanapoendelea kuchakarika katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na udugu; mambo msingi yanayoendelea kufanyiwa kazi na Serikali ya Colombia, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani na maridhiano kati ya watu vinatawala ili hatimaye, kuondokana na kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia ambacho kimeendelea kusikika miaka nenda miaka rudi!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, anaitaka Familia ya Mungu nchini Colombia kuwa ni  mashuhuda wa Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwani Yesu Kristo ni chemchemi ya furaha na amani ya kweli; anayeweza kuwatuliza na kuwafariji wote wanaoteseka kutokana na ukosefu wa misingi ya haki na amani. Waamini wanahimizwa kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki na amani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo kwa Mungu na jirani; kwa kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi; haki, udugu, mshikamano, majadiliano pamoja na maridhiano ndani ya jamii. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa ujenzi wa maisha ya jamii yaliyopyaishwa.

Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wa Colombia kusimama kidete kupinga mambo yote yanayowanyima watu haki zao msingi; ukosefu wa misingi ya usawa, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma na utengano. Haya ni mambo ambayo kimsingi yanameng’enyua mfungamano na mshikamano wa kijamii. Ujenzi wa misingi ya amani ya kudumu unahitaji watu kujikita katika utu na heshima ya binadamu; kwa kutambua na kuguswa na mahangaiko ya wengine; kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato pamoja na kuhakikisha kwamba, wananchi wote wanashirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa nchi yao kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mchakato wa ujenzi wa amani ya kudumu unajikita pia katika maboresho ya mahusiano ndani ya familia, ili kweli ziweze kuwa ni mashuhuda amini wa shule  na utamaduni wa haki, amani, upatanisho na maridhiano. Wananchi waendelee kuwasaidia waathirika wa mabomu ya kutegwa ardhini, watu wasiokuwa na makazi maalum bila kuwasahau watu waliokuwa wametekwa nyara kwa muda mrefu, wakanyanyasika na kudhalilishwa utu na heshima yao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki Colombia kulitumia Kanisa kuwa ni mahali pa kutibu na kuganga madonda yaliyojitokeza katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Colombia kiasi cha kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya watu wengi. Kanisa liwe ni mahali pa watu kuona tena maana ya maisha na utu wao; mahali pa kuomba na kupokea msamaha, tayari kuanza maisha mapya yanayojikita katika haki, amani na ukweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.