2015-04-04 11:41:00

Kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia kinaendelea kusikika Kenya!


Damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika nchini Kenya kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa kwa misingi ya udini, usiozingatia zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwenye haki sawa kama wengine ndani ya jamii. Hivi karibuni, Kardinali Angelo Bagnasco wakati akifungua mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia alisikitishwa sana na ongezeko la vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, mauaji yanayofanywa kwa kisingizio cha misimamo mikali ya kiimani na walengwa wakuu wa ni Wakristo!

Kenya ni nchi ambayo inakaliwa na waamini wa dini na makabila mbali mbali, lakini katika miaka ya hivi karibuni kuna baadhi ya watu wamethubutu kuwagawa wananchi wa Kenya kwa misingi ya udini na ukabila; mambo ambayo kwa sasa hayana mvuto wala mashiko. Mauaji ya wanafunzi 147 huko Garissa yanaendelea kutonesha madonda ya mauaji na ubaguzi wa kidini yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi hivi karibuni na kusababisha watu 68 kupoteza maisha yao.

Ni mashambulizi yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kutoka Somalia ambako uhuru wa kidini umekufa kifo cha kawaida na wala hakuna tena utawala wa sheria, hapa kinachotawala ni falsafa ya mwenye nguvu mpishe! Lakini hii si haki, kwani tofauti za kidini kisiwe ni chanzo cha vita, vurugu na kinzani za kijamii na badala yake, tofauti hizi ziwe ni msingi wa kukoleza amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Shirika la Kipapa la Msaada kwa Makanisa hitaji, ACS, linasema kwamba, linasikitishwa sana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa misingi ya kidini. Tangu mwaka 2012, Shirika hili limekuwa likishirikiana kwa karibu sana na Jimbo Katoliki la  Lodwar ili kuhamasisha majadiliano ya kidini, ili kujenga misingi ya haki na amani, kwani eneo hili pia limekuwa likitikiswa kwa mapigano ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima.

Elimu, mawasiliano na majadiliano ya kidini ni kati ya mambo msingi yanayofanyiwa kazi kati ya Shirika la Kipapa la Msaada kwa Makanisa hitaji na Jimbo Katoliki la Lodwar, ili kusaidia mchakato wa upatanisho kati ya wananchi wanaoishi kwenye mpaka wa Kenya na Somalia, eneo ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa ni uwanja wa fujo na ghasia.

Askofu Dominic Kimengich wa Jimbo Katoliki la Lodwar, Kenya anabainisha kwamba, Jimbo lake linaendelea kuwekeza katika majiundo endelevu na majadiliano kati ya wananchi ndani na nje ya Kenya. Ni majiundo ya kina katika ukweli na uwazi, kwa kujali na kuheshimu utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi yanaweza kusaidia kusitisha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.