2015-04-04 14:14:00

Je, kwanini kuna mateso na kifo?


Swali kubwa ni hili – kwa nini Mungu ameruhusu mateso? Nabii Ayubu – 31:37 – anapoongelea kuhusu mashindano ya mwisho anaomba Mungu ampe majibu. Jibu halionekani katika kitabu hiki cha Ayubu ila kinachoonekana ni kuwa fumbo la mateso lamezwa katika fumbo kuu la upendo la Mungu mwenyewe. Kwa namna ya pekee, imani ya kikristo inaliishi fumbo hili – upendo mkuu wa Mungu. Haitoi jibu la moja kwa moja ni kwa nini ni kwa njia ya mateso ila twapata maelezo mbalimbali jinsi Mungu anavyotumia njia ya mateso kumkomboa mwanadamu. Mungu hutumia mateso ya mwanadamu ili kumkomboa mwanadamu. Lakini Fumbo labaki.

Wainjili wetu wanaeleza historia ya mateso ya Yesu na kifo, lakini hawatoi jibu ni kwa nini lazima Yesu apitie njia ya mateso ili kutupatia wokovu. Ila wanaeleza matokeo yake kwamba kinachopatikana ni wokovu – matokeo ya mateso na kifo chake Kristo. Yaani matokeo yake ni wokovu wa mwanadamu. Mwinjili Marko – Mk. 15:39 – anasema tendo la kifo cha Yesu ndiyo sababu ya imani ya yule Akida – basi yule akida aliyesimama hapo alimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Mwinjili Matayo – anaona ufufuko katika kifo cha Yesu – Mt. 27:52-53 – makaburi yakafufuka, ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala. Nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.

Mwinjili Yohane – Yoh. 19:30 – analinganisha kufa kwa Kristo na kutupatia roho – basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, imekwisha, akainama kichwa, akaisalimu roho yake. Mwinjili Yohane - Yoh. 19:34-37 - ila askari mmoja wapo alimchoma ubavu kwa mkuki mara ikatoka damu na maji aliyeona hayo ameyashuhudia na ushuhuda wake ni kweli naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi pia mpate kusadiki maana hayo yametendeka ili andiko litimie lisemalo hautavunjwa mfupa hata mmoja. Tena andiko lingine lasema watamtazama yule waliyemchoma.

Mt. Paulo naye anaendelea kusaidia kutoa majibu anapowaandikia Wafilipi katika 2:6 ...akiwaambia hivi: mwatakiwa kuwa wapole na wanyenyekevu na kuwa na mtazamo wa Kristo. Naye Kristo anaonesha wazi hilo – anajishusha na kuwa mwanadamu hata kufa msalabani.

Habari juu ya mateso ya Kristo iko wazi katika maandiko matakatifu. Ushuhuda wa imani anaotoa Mt. Petro juu ya ufuasi uko wazi katika fundisho la Yesu juu ya msalaba – Mk. 8:34-38 – mtu akitaka kuwa mfuasi wangu, ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake .... . Fundisho hili la imani linakamilishwa na maneno ya Yesu mwenyewe – ye yote yule anayetaka kunifuata ni lazima achukue msalaba wake na anifuate

Pia tunaona Marko na Paulo – wanasisitiza haja ya kukubali mateso ili kukamilika katika maisha ya Kikristo. Ila wanaweka wazi kuwa hili si jambo la kibinafsi tu. Wote wanatambua kuwa katika Kristo hupatikana ukamilifu. Yesu kadiri ya Marko na Paulo ni zaidi ya mwalimu anayeongoza wengine tu. Anayefundisha watu ili wapate kuwa hai. Yesu ni uhai wenyewe, ni chanzo cha nguvu yetu sisi ya kumfuata yeye.Ukiangalia kwa umakini wimbo kwa Kristo katika Waf. 2:6.... wimbo wazungumza habari ya umungu wake, anayejitoa kabisa na kuchukua aina ya mtumwa. Na baadaye kutukuzwa kwake mbinguni na kupewa jina la Bwana.

Mwanazuoni mmoja anaandika hivi – ni nani ambaye angeweza kufanya hivyo? Mfano wa Kristo kujitoa kabisa ulifanywa ili kutoa wokovu. Kwa vile alifanya alichofanya, sisi twaweza kufanya anachotaka sisi tufanye.  Tunaalikwa tuige mfano wa mtumishi mtii anayeteseka. Ndicho tunachoambiwa pia leo. Lakini zaidi twaambiwa kuwa katika Kristo tunayo nguvu ya kuteseka. Kwa kumpokea yeye, tunapokea nguvu ya kufanya kama alivyofanya yeye. 

Tutafakarishwe na mfano huu: Ndugu wawili – mdogo alikuwa jambazi na kila aina ya maisha ya ubaya na yasiyofaa kwa jamii. Kaka mkubwa daima alikuwa akitumia kila aina ya ushawishi na maonyo ili ndugu yake aondokane na maisha hayo ya ujambazi. Usiku mmoja huyu ndugu mdogo jambazi akarudi nyumbani mbio na nguo zake zimejaa damu. Mara akamwambia kaka yake nimeua mtu. Lakini mimi sitaki kufa. Dakika chache baadaye nyumba ikawa imezingirwa na polisi. Wote wawili wakajua wazi kuwa hakuna namna yo yote ile ya kutoroka katika mikono ya askari. Yule ndugu jambazi akaanza kulia sikunuia kumuua yule. Mimi sitaki kufa. Alimwambia kaka yake. Kaka mtu akapata wazo. Akachukua nguo za yule ndugu yake jambazi na kuzivaa. Polisi walipoingia ndani wakamkamata, wakamshtaki na kumhukumu kufa kwa sababu ya kuua. Akafa yeye na ndugu yake akabaki. Alikufa kwa ajili ya ndugu yake. Hiki ndicho anachofanya Yesu kwa ajili yetu. Leo tunaadhimisha tendo la la mapendo – upendo wa Mungu kwetu. Sisi tutalipaje upendo huo? Yule ndugu mdogo atalipaje upendo kwa kaka yake aliyekufa badala yake?

Ndugu wapendwa, ni lazima majibu ya maswali yetu yapatikane katika maandiko matakatifu. Jibu la kidunia kuhusu kifo ni huzuni, karaha, wasiwasi, mashaka, kilio n.k. Jibu la Mungu ni tofauti. Ni furaha, ni utukufu, ni uzima mpya. Mbegu isipoanguka na kuchipua, haitazaa. Ni ajabu kweli. Nabii Ayubu anatuambia, mateso yanapoteza uzito wake yanapohusishwa na upendo wa fumbo la Mungu. Peke yetu hatutaweza kuelewa fumbo zito la ukombozi wetu. Ni katika imani tu twaweza kupata jibu. Mtazamo wa haya tufanyayo upo mbele, kwake Mungu. Hatuwezi kufanya mambo yamhusuyo Mungu na kutaka kupata majibu hapa hapa au hapo hapo au jinsi tunavyofikiri au kutaka sisi. Sisi kama tunamwamini Mungu, tumempokea Yesu, basi tuenende kadiri ya amri na maagizo yake na tumpe nafasi atende kazi yake ndani yetu.

 Mtume Paulo anaandika –  maana niliazimu nisijue neno lo lote kwenu, ila Yesu Kriso, naye aliyesulubiwa – 1Kor.2:2. Msalaba una siri ya ajabu. Yesu Kristo analaaniwa juu ya mti, ili sisi tupate kuepa laana, pale msalabani – Mungu Mwenyezi kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, alihukumu dhambi katika mwili – Rom. 8:3.

Binadamu kwa vile tumemwasi Mungu kwa dhambi za kijumuiya na kwa dhambi za kibinafsi tulikuwa na hati ya mashtaka inyotuhukumu kupotelea mbali, lakini Kristo amefuta hiyo hati iliyoandikwa ya kutushtaki kwa hukumu zake iliyo na uadui kwetu, ameiondoa isiwepo tena, ameipigilia msalabani – Kol. 2:14. Hii ndiyo siri ya msalaba. Hii ndiyo sababu kuu ya kuabudu msalaba mtakatifu wa Bwana Wetu Yesu Kristo, mwokozi wa ulimwengu.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.