2015-04-03 15:32:00

Shambulio la kigaidi Garissa ni unyama usioelezeka


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, kupitia Katibu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin, alipeleka salaam zake za rambirambi kwa  Wakenya wote kufuatia  shambulio la kigaidi, lilillofanywa na wanamgambo wa al Shaabab katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya, mapema  siku ya Alhamisi Kuu. Rambi rambi hizo alizozituma kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ,  Kardinali John Njue, amesema shambulio hilo  ni ukatili usiokuwa na maana yoyote. Katika shambulio hili, watu 147 wamethibitishwa kufariki na mamia mengine kubaki majeruhi. Inatajwa walengwa hasa ilikuwa ni wanafunzi Wakristo.

Papa masikitiko mengi ameungana na Wakenya katika kuomboleza vifo vilivyotokea, na anawatakia wapate ahueni haraka waliobakimajeruhi. Amelaani vikali mauaji ya watu wasiokuwa na hatia .Na kwa masikitiko makubwa , ametoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea uongofu wa moyo wahalifu hao. Amewaaka Wakenya wote washiriki katika jitihada za kukomesha vurugu. Na kila mtu aongeze kasi katika kujenga upya udugu ,haki na amani. Na pia ameitaka jumuiya ya kimataifa kutenda kwa nguvu zaidi kupitia Umoja wa Mataifa. Kuchukua hatua kali zinazostahili kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa raia na kuzuia matendo maovu kama hayo kamwe yasitokee. 

Na Padre Nicholas Mutua ,Mkuu wa tume ya Haki na amani katika Jimbo Katoliki la Garissa , ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria ya Garissa, akihojiwa na Redio Vatican, juu ya tukio hili, amesema  ni unyama wa hali ya juu  uliofanywa na watu hao  waliopoteza dhamiri yao kama binadamu.Watu hao wanaosema  wanataka kueneza dini ya Kiislamu si watu wa Mungu, maana hata Koran huwataka Waislamu kuheshimu maisha ya watu wote wakiwemo Wakristo. Na kwamba  shambulio hili lilifanyika kwa kasi kubwa. Na kwa  sasa Chuo Kikuu cha Garissa kicho chini ya vikosi vya ulinzi na usalama nchini Kenya. 

Padre Mutua ameendelea kuizungumzia hali ya wakati huu katika eneo hilo la Garissa kwamba,watu wote wamegubikwa na woga na wasiwasi mkubwa maana hawajui lini wanaweza vamiwa na  wanamgambo hao wa al Shabab. Watu hawana uhakika na usalama wao hata wanapokuwa mitaani katika harakati za kuendesha shughuli zao . Na kwamba si Wakristo peke yao wanaoshambuliwa, ametoa mfano wa Imamu aliyekuwa anamfahamu, alishambuliwa na kuuawa kwa kuwa hakukubaliana na unyama unaofanya wanamgambo hao Pia anasema Wakristo hawawezi kuondoka na kuiacha nchi yao ya Kenya. Wataendelea kubaki katika eneo lao na kuendelea kuishuhudia Injili ya Upendo wa Kristo. Wataendelea na  jitihada za kujaribu kupandikiza mbegu ya amani kwa watu hao, kama Papa Francisko anavyo himiza mara kwa mara ,kujenga uvumilivu, kutokuwa watu wa  kupiza kisasi , lakini kuwa watu wa majadiliano .Na si kujenga utengano lakini Umoja. Padre Mutua ameoneysha kutambua kwamba,Baba Mtakatifu daima yu karibu na watu wa Afrika, hasa wnaoteseka kutokana na imani yao kwa Kristo. 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.