2015-04-03 09:04:00

Papa asema: Ni upendo unaohudumia, okoa na kusafisha


Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Karamu ya Mwisho, Alhamisi jioni, 2 Aprili 2015, siku ile iliyotangulia mateso ya Kristo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Gereza kuu la Rebibbia lililoko mjini Roma na kuwaosha miguu wafungwa 12 wanaotumikia adhabu gerezani humo. Mfungwa mmoja wa kike pamoja na mtoto wake alitokwa na machozi ya uchungu pale alipomwona Baba Mtakatifu akiinama na kumwosha miguu mtoto wake mdogo na baadaye kuipangusa na kuibusu! Pengine, hili ni tukio litakaloacha chapa ya kudumu katika maisha ya mama huyu kutoka Nigeria.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu upendo ulioneshwa na Yesu wakati wa Karamu ya mwisho, kwani aliwapenda upeo na bado anaendelea kuwapenda watu wake na kamwe hachoki kupenda pasi na ubaguzi. Yesu alionesha upendo wa hali ya juu kiasi cha kujisadaka pale juu Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, amemkomboa mwanadamu kwa upendo unaojionesha katika uhalisia wa mtu binafsi, akiwa na majina yake kamili.

Upendo wa Yesu anasema Baba Mtakatifu, kamwe hauwezi kudanganya, kamwe hachoki kupenda, kusamehe na kukumbatia! Yesu aliwaonesha wafuasi wake jinsi ya kupenda kwa kujisadaka na kwa njia ya huduma makini kama walivyokuwa wanafanya watumwa enzi zile. Yesu aliamua kuwaosha mitume wake miguu, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa; upendo unaohudumia, okoa na kusafisha.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linaendeleza utamaduni huu wakati wa Ibada ya Misa ya Ekaristi Takatifu, Alhamisi jioni, kwa kuwaosha miguu waamini 12 kielelezo cha Mitume wa Yesu, kinachoiwakilisha Familia yote ya Mungu. Anawaosha na kuwatakasa ili waweze kuonja tena upendo wake usiokuwa na mipaka; huu ndio upendo wa Mungu unaodumu daima. Baba Mtakatifu anasema, hata yeye anahitaji kuoshwa na Yesu, kumbe, amewaomba wafungwa hao kuendelea kumwombea, ili aweze kujisadaka na kuwa ni mtumishi wa wote, kama ilivyokuwa kwa Yesu.

Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko aliwashukuru na kuwatakia wafungwa wote maadhimisho mema ya Juma kuu na hatimaye, Pasaka ya Bwana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.