2015-04-03 09:43:00

Ni kwa wale tu walioguswa ndio wanakimbilia Makaburini! Kulikoni?


Ni ajabu iliyoje kuona heshima kubwa inayotolewa kwa marehemu. Marehemu wa kiume ataveshwa suti maridadi na ya gharama na kuonekana kama Bwana arusi aendaye kufunga ndoa au kama mhadhiri aendaye kutoa mhadhara. Marehemu wa kike atapambwa vizuri kama bi arusi. Marehemu akiwa Padre au askofu huyo ataveshwa nguo za ibada kama vile anaenda kuadhimisha Misa Takatifu au kutoa sakramenti ya upadre. Marehemu akiwa mtawa kadhalika, atavishwa vazi rasmi la ibada wanaloliita “kanzu ya korus.” Baada ya kuandaliwa vizuri hivyo, marehemu atalazwa kwenye jeneza zuri na watu watakuja kumuaga na kumpa heshima za mwisho, ikifuatiwa na ibada ya kumtakia kila la heri ya huko aendako ikiwa ni pamoja na kumsalia Misa Takatifu au ibada nyingine ya kidini, kama vile ingekuwa sikukuu ya “send off".  Kishapo marehemu anapelekwa kwa heshima kwenye makao ya milele yaani makaburini kama vile angesindikizwa kwenda reception. Huko makaburini nako, kuna madhehebu yake mengi ikiwa ni pamoja na kumtolea hotuba mbalimbali za wasifu na kupamba kaburi kwa maua mazuri na mishumaa. Baadaye wazikaji na wote waliohudhuria mazishi wanakunywa uji, ingawaje kwa kweli ni kula na kunywa kabla ya kutawanyika.

 

Katika historia kumekuwa pia mataifa pamoja na makabila mengi yenye tamaduni tofauti wa kuhesimu na kumhifadhi marehemu. Mtu unabaki kujiuliza: Ni msiba au sikukuu? Madhehebu hayo yote yana maana gani kwa marehemu? Kwa sababu sote tunaelewa kwamba marehemu huyo ataishia kugeuka kuwa udongo na mavumbi. Kulikoni basi kuingia gharama kubwa ya kumhadaa marehemu kiasi hicho, au labda kuna maana ya pekee iliyofumbika machoni na akilini mwetu na tunashindwa kueleza kwa lugha ya kawaida. Ili kupata majibu kwa maswali hayo, na kutusaidia kueleweza fumbo lililojificha katika madhehebu tuwafanyiayo marehemu wetu wakati wa mazishi, ninakualika kutafakari juu ya mazishi ya Yesu kwa nafasi hii ya sikukuu ya Pasaka ya Bwana wetu.

 

Katika mazishi ya Yesu kulikuwa pia na maandalizi mazuri ya mwili wake kama vile angeenda arusini. Mwinjili Yohane anawataja watu wawili maarufu waliohusika kuandaa mwili wa Yesu na kuuzika. Nao ni Yosefu wa Arimatea na Nikodemu yule aliyeenda kuteta au “kunong’ona” na Yesu usiku. Nikodemu alifika na manemane ya kupaka maiti pamoja na udi (ubani) ili kuifukizia harufu nzuri maiti na kaburi atakalozikwa. Yasemwa kuwa manemane hayo pamoja na harufu nzuri ya udi (ubani) vilikuwa vinatumika pia kuwapaka wanaarusi na kufukiziwa chumba rasmi cha wana arusi wapya siku ya kufunga ndoa. Baada ya kuuandaa mwili wa Yesu wakauzika kwa heshima katika kaburi jipya. Ilikuwa siku ileile ya ijumaa aliyokufa, na walizika kwa harakaharaka kwa sababu siku ile ilikuwa ni jioni ya kuanza sherehe za sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi iliyofuata siku ya Sabato (Jumamosi).

Tunashuhudia jinsi Yesu waliyemheshimu na kumthamini sana, jinsi walivyomwandaa kama bwana arusi, wanamlaza katika kaburini jipya, kisha wanaenda kwenye sikukuu ya Pasaka. Toka hapo Mwinjili ananyamaza, na hasemi kilichotokea siku ya sabato. Maana yake, siku hiyo ambayo Mungu alipumzika kufanya kazi ya uumbaji, ilikuwa kama siku ya kila mmoja kutafakari na kujihoji moyoni kilichotokea. Kwa vyovyote hali iliyowakumba wapendwa wa marehemu siku ile ya ijumaa, jumamosi hadi jumapili asubuhi ni uchungu, upweke, woga, wasiwasi vinavyowakilishwa na neno hili giza. Hivi zilikuwa ni siku za giza nene. Kila kitu kilibaki kimesimama au kimekufa ganzi.

 

Watu wamepumbazika, wanajiuliza maswali yasiyo na majibu, na baadaye wanaishia kuguna: “Kulikoni kumetokea mambo haya. Kwa nini Mungu hajaliingilia kati suala zito kama hili.” Pindi wakiwa katika giza la msiba na kufa ganzi hadi siku ya tatu, mioyo ya waliompenda Yesu ilishindwa kutulia na kusahau kilichotokea. Ama kweli “maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo.” Kwa hiyo, siku ya tatu upendo unaanza kuchukua hatua, yasemwa: “Hata siku ya kwanza ya juma, mtu wa kwanza tena mwanamke, anajitokeza hadharani, yaani Maria Magdalena anakwenda kaburini peke yake, alfajiri, kungali giza bado.” Neno hili “kaburini” linanukuliwa mara saba ili kuonesha kuwa hiyo ni hatima ya binadamu wote, kwamba mbele ya kaburi binadamu hatuna ujanja. Na “giza la asubuhi” yaani giza nene la uchungu, wasiwasi na woga unaowakumba hata wanaume, hapo unakutana na mwanamke asiye na woga kwa sababu moyo wake umependa mno anachomoka peke yake usiku tena kwa haraka anakwenda kaburini.

 

Haitolewi hoja kwa nini mwanamke huyu anaenda kaburini bila kitu chochote mkononi kama ilivyokuwa kwa wanawake wengine. Yeye analo moja tu moyoni mwake nalo ni upendo unaogoma kabisa kuelewa kuwa Yesu aliye upendo amekufa. Aidha katika masimulizi ya Pasaka, wote wanaoenda na kufika wa kwanza kaburini asubuhi ile ni wale tu walioguswa kwa hali ya juu sana na nguvu ya upendo kwa Yesu. Watu hao ni Wanawake, Maria Magdalena, na Mwanafunzi aliyempenda sana Yesu. Ni watu hawa pekee yao ndiyo waliokuwa wa kwanza kuelewa upendo mkubwa kama ule wa Yesu, upendo ambao wanaona usingeweza kufutika hivihivi tu kirahisi eti kutokana na kifo. Ama kweli “Kipenda roho ni dawa.”

 

Maria Magdalena afikapo kaburini anaona jiwe limeondolewa na kaburi liko wazi. Hapo mara moja, anajua kuna jambo lisilo la kawaida limetokea. “Anaondoka mara na kwenda mbio kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine.” Halafu bila kujitambua anawalopokea maneno ya imani na upendo mkubwa bila kujitambua mwenyewe: “Wamemwondoa Bwana.” Badala ya kusema “wamechukua maiti, anasema “Bwana…” kama vile angekuwa bado hai. Kwa taarifa hii, Maria Magdalena anawaunganisha tena wanafunzi waliokuwa wametawanyika baada ya kifo cha Yesu, aidha anawawakilisha wanafunzi wanaompenda Kristo, yaani wale walio katika giza la uchungu wa mateso na mauti, lakini wanaendelea bado kumtafuta mpendwa wao wakiwa na uhakika kwamba hawezi kuwaacha.

Mbiombio alizoanzisha Maria Magdalena kutokana na upendo, anawaambukiza hata wanafunzi, kwani anapowataarifu tu “Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili, bali mwanafunzi yule mwingine alikimbia mbio zaidi ya Petro. Yule mwanafunzi, aliyempenda zaidi Yesu anakimbia haraka zaidi na kufika wa kwanza kaburini.” Kutokana na kupenda zaidi anakuwa wa kwanza kuelewa mambo kwa urahisi na kusadiki, kwa sababu anayependa au anayependwa zaidi anaelewa mambo kwanza na kwa undani zaidi. Kwa vyovyote mwanafunzi huyu asiyejulikana jina – (lakini baadaye yasemwa alikuwa ni Yohane mwana wa Zebedayo) – mwanafunzi huyo anamwakilisha kila mmoja wetu. Kutokana na upendo wake anatuonesha njia ya kufuata katika imani.

 

Mwanafunzi huyu alipofika kaburini, “Anainama na kuchungulia, anaviona vitambaa vya sanda vimelala, lakini hakuingia.” Hapa kuna neno hili “kuona” (plebo) kama kuona kule kwa kawaida alikoona Maria Magdalena. Hii ni alama ya jumuia yaani kutofautiana katika kuona na kupata imani. Wengine wanaona na kuwa na imani mara moja, lakini wengine inawachukua muda hadi kuelewa. Kisha hapo, “akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwa kichwani pake, haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali pa peke yake, akaamini.” Hapa “kutazama” kwa Petro kumetumika neno la Kigiriki “theoreo” lenye maana ya kuangalia na kufanya tafakari. Alama zote zionekanazo hapo kwa macho ya kawaida ni za kifo naye anazifanyia tafakari (theoreo). Hadi hapa tumesikia tu neno kuona kwa kawaida (plebo) kwa mwanafunzi aliyependwa zaidi pamoja na kule kwa Maria Magdalena na wameamini.

 

Lakini Petro yeye ameanza kufanyia tafakari (theoreo). Halafu, “basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini.” Hapa sasa “kuona” kwa Yohane kunatumika orao. Neno hilo orao litumikapo wakati wa pasaka laonesha mtazamo tofauti, siyo mtazamo wa kawaida unaoweza kuainisha kwa maneno, bali ni mtazamo wa imani. Mwanafunzi huyu asiyejulikana jina mwenye upendo zaidi, anaingia ndani ya kaburi na mtazamo tofauti wa kifo. Aidha, haisemwi kwamba mwanafunzi huyu alianza kumsadikisha Petro kwamba Yesu amefufuka, la hasha, bali alikuwa na mtazamo binafsi ambao ni vigumu kumsadikisha mwingine. Kwani wanachoona wote, ni vitambaa na sanda. Lakini vitu hivyo sivyo vithibiti vya ufufuko. Mtu mwenye upendo anaona tu na kuamini, na wengine wanaamini hata bila kuona. Hayo ndiyo mang’amuzi tunayoweza kuwa nayo kwa mtu tunayempenda.

 

Kadhalika kwetu sisi, tunachoona (plebo) watu wote tukiwa msibani, ni maiti iliyoveshwa safi, tunaona jeneza na kaburi lililopambwa. Lakini mwenye upendo ataona orao kwa jicho tofauti. Huo ni mwono ambao wasio na imani na upendo hawawezi kuwa nao. Je wewe unaona nini unapomtazama maiti aliyeveshwa vizuri kama anaenda kwenda sikukuu? Hapo kila mmoja atakuwa na jibu la peke yake kutokana na namna anavyoangaia. Angalia jinsi Mwinjili anavyohitimisha ili kutusaidia kutafakari jambo hilo aposema: “Kwa maana hawajalifahamu bado Andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.”

 

Ndugu zangu, sikukuu ya Pasaka tunaitwa kuishi imani yetu. Mungu ametupatia uwezo huu wa kuangalia na kuelewa ukweli huu kwa jicho la upendo. Tunaalikwa kutafakari juu ya maana ya maisha yetu. Kila kitu kinaweza kupata maana endapo tunakitazama kwa mwanga wa Pasaka. Hapo uchungu wa msiba  unakuwa na matumaini ya furaha ya Sikukuu ya kufufuka na Bwana! Heri kwa Sikukuu ya Pasaka!

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.