2015-04-03 07:42:00

Mapadre 10 wapata chakula cha mchana na Baba Mtakatifu Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kubariki mafuta ya Krisma ya wokovu yatakayotumika kwa ajili ya maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali katika kipindi cha mwaka mzima, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi tarehe 2 Aprili 2015, amewataka Mapadre kujisadaka hadi kupata mchoko mtakatifu, jambo linalompendeza Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko amewataka Mapadre pia kutambua jinsi ya kupumzika baada ya kuchoka katika kuwahudumia Watu wa Mungu, bila kujitumbukiza katika malimwengu. Mapadre watambue kwamba, watu wanataka kuwaona Mapadre wakiwa kati yao kwa ajili ya huduma ya Neno na Sakramenti, huu ndio mchoko mtakatifu “anaoufagilia” Baba Mtakatifu. Mapadre watambue jinsi ya kupambana na changamoto za maisha na wito wa kipadre. Yesu anawataka wafuasi wake kuwa na ujasiri kwani Yeye ameushinda ulimwengu.

Mapadre wasiwe na kishawishi cha kuchoka kiasi hata kutamani “kubwaga manyanga” ya maisha na wito wa Kipadre. Yesu daima yuko tayari kuwasafisha, kuwaganga na kuwaponya madonda yao, wanapomkimbilia kwa upole na unyenyekevu. Yesu anawataka Mapadre kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha na Matumaini, kwani daima yuko pamoja nao, hadi utimilifu wa dahali.

Baada ya Ibada ya Misa ya kubariki Krisma ya wokovu, Baba Mtakatifu Francisko alipata chakula cha mchana na Mapadre kumi kutoka Jimbo kuu la Roma, Mapadre wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu katika shughuli mbali mbali za kichungaji. Kwa muda wa saa moja na nusu, Baba Mtakatifu alizungumza na kubadilishana mawazo na Wakleri wenzake. Lengo la Baba Mtakatifu ni kutaka kufahamu zaidi maisha na utume wa Wakleri pamoja na changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo.

Baba Mtakatifu amesikiliza kwa makini shuhuda mbali mbali zilizokuwa zinatolewa na Mapadre hawa na amewabariki na kuwatia moyo kusonga mbele pasi na kukata tamaa. Hapa Baba Mtakatifu pamoja na Mapadre wenzake wamejipatia fursa ya mapumziko ya kiroho kwa kupata chakula pamoja na kubadilishana mawazo, jambo ambalo linapendeza mbele ya Mungu na wanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa,

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.