2015-04-03 11:18:00

Kenya itawasaka na kuwashikisha adabu magaidi waliohusika na mauaji


Serikali ya Kenya imesema kwamba, kamwe haitakubali kupigishwa magoti na magaidi wanaotaka kuvuruga misingi ya haki, amani, utulivu na maridhiano kati ya watu na badala yake, Serikali itahakikisha kwamba, “inakula na magaidi sahani moja hadi kieleweke”. Hayo yamesemwa na Bwana Joseph Nkaissery, Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Kenya kufuatia shambulizi la kigaidi lililosababisha wanafunzi 147 kuuwawa kikatili na baadhi yao hadi sasa hawajulikani waliko.

Inahofiwa kwamba, pengine wametekwa nyara na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kutoka Somalia. Waziri wa mambo ya ndani ya nchi anasema kwamba, shambulizi lililofanyika huko Garissa kwa kufanya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia linalenga kudhohofisha Serikali, lakini Serikali imeamua kwamba, itapambana nao hadi kieleweke. Shambulizi dhidi ya Chuo kikuu cha Garissa ni kati ya mashambulizi mabaya yaliyowahi kufanywa na kikundi cha kigaidi tangu mashambulizi kama haya kutekelezwa na kikundi cha Al Qaeda kwenye Ubalozi wa Marekani nchini Kenya na kupelekea watu 213 kupoteza maisha yao.

RAM.








All the contents on this site are copyrighted ©.