2015-04-03 11:42:00

Hija ya mshikamano na upendo kwa Wakristo nchini Iraq


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu bado anaendelea na hija yake ya kitume nchini Iraq ambako anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa kidugu na Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika huko kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Akiwa nchini Iraq ametembelea na kuzungumza na wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaohifadhiwa kwenye kambi za wakimbizi.

Kardinali Filoni amebahatika kuzungumza na viongozi wa Kanisa, watawa pamoja na wafanyakazi wanaowahudumia wakimbizi na kuwatia shime kusonga mbele kwa imani na matumaini na kwamba, Kanisa linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati. Kardinali Filoni amezungumza pia na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini ya Kiislam, lakini muda mwingi ameutumia kuzungumza na wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Hali kwa sasa inaonekana kuwa shwari kidogo ikilinganishwa na mambo yalivyokuwa mwezi agosti 2014. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, familia nyingi zimeanza kupata makazi ya muda, ingawa hali bado ni tete sana. Kardinali Filoni amewasilisha pia zawadi ya Pasaka kutoka kwa waamini wa Jimbo kuu la Roma kama kielelezo cha upendo na mshikamano wao wa kidugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.