2015-04-03 09:22:00

Alhamisi Kuu - Papa aosha miguu ya wafungwa


(Vatican Radio) Papa Francisko  Alhamisi jioni, aliadhimisha Karamu ya Mwisho ya Bwana, akiwa katika gereza la Rebbibia jijini Roma. Misa uliohudhuriwa na wafungwa wanaume na wanawake wa  gereza hilo. Katika Ibada hii , Papa Francisco aliosha miguu ya wanaume sita na wanawake  sita, ikiwa ni pamoja mama mmoja aliyekuwa ameshika mtoto wake mdogo .

Homilia ya Papa katika Ibada hii ililenga katika  Injili  inayosema “Aliwapenda walio  wake  duniani , na aliwapenda mpaka mwisho." Papa alifafanua kwamba, maneno haya yanatuambia leo hii sisi waamini wake kwamba,  anatupenda bila mipaka, anatupenda mpaka mwisho.  Na kamwe hachoki kupenda . Anatupenda sisi sote kiasi cha kuyatoa maisha yake sadaka , kwa ajili ya kusafisha dhambi zetu , ili tupate stahili ya kuitwa wana wa Mungu na kuwa warithi wa maisha ya milele.  Baba Mtakatifu alieleza na kumgeukia kila mfungwa mmoja mmoja akisema, Yesu alitoa uhai wake nkwa ajili yako na  kwa ajili yangu na kwa ajili ya kila  mtu,  huku  akimtaka kila mmmoja kutaja jina lake la kwanza na la  mwisho. Upendo wa Yesu ni kamili tena binafsi.


Papa aliendelea na homilia kwa kufanya nukuu kutoka Kitabu cha  Isaya, "upendo wa Mungu hauna mipaka. Hata kama mama anamsahau mtoto wake, mimi s kamwe sitakusahau wewe", alirudia maneno hayo na kuhakikishia wafungwa kwamba,  hivyo ndivyo ulivyo  upendo wa Mungu kwetu.

Wakati Baba Mtakatifu akiinama kwa nia ya kuwaosha miguu wanawake sita na wanaume sita, baadhi ya wafungwa waliguswa na tendo hilo na kutoa machozi na ukelele wa mshangao ,  Papa ameosha miguu yangu, .  Kati ya wafungwa hao alikuwa ni Mwanamama mmoja mfungwa aliyekuwa na mtoto wake , ambaye Papa pia aliosha miguu ya mtoto huyo mdogo.

 Mapema kabla ya tukio hili la kuwaosha miguu Papa alieleza asili yake kwamba , wakati wa Yesu watu walikuwa wakitembea kwa miguu. Hapakuwa na magari kama wakati huu . Na hivyo walikuwa na mila ya kunawisha miguu kabla hawajaingia ndani ya nyumba , maana miguu  ilikuwa inachafuka kwa vumbi la njiani. Na hivyo  walinawa miguu , lakini kazi hiyo ya kunawisha  miguu, haikufanywa na mkuu wa nyumba bali ilifanywa na mtumwa. Yesu alifanya kazi hiyo ya watumwa , ingawa yeye alikuwa ni Bwana , kutokana na  upendo wake. Na hivyo akawa mtumwa wa kututumikia, kutuponya, kutusafisha.

Papa Francisco, kwa unyenyekevu alionyesha hamu yake kubwa ya kutaka kuoshwa miguu yake na Bwana. Alisema, na kwa ajili hii, wakati wa Ibada hii, namwomba Bwana  asafishe kila kosa nililofanya, kila doa la dhambi , ili pia niwe mtumwa  katika utumishi wangu, kuwatumikia watu kama alivyofanya Yesu.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.