2015-04-02 10:09:00

Tafakari ya Ijumaa kuu: Njia ya Imani, Njia ya Mshikamano


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika maadhimisho ya Ijumaa kuu, Siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, limeandaa tafakari ya Njia ya Msalaba inayogusa shida, mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya kati na katika Nchi changa zaidi duniani, ili kuwasaidia waamini kumwona Kristo anayeteseka kati ya watu wake sehemu mbali mbali za dunia.

Njia hii ya Msalaba inaongozwa na kauli mbiu “Njia ya Imani na Njia ya  Mshikamano”. Kwa namna ya pekee, Maaskofu Katoliki Canada wanaangalia changamoto zinazowakabilia Wakristo huko Mashariki ya Kati kutokana na ukosefu wa amani, utulivu na maridhiano kati ya watu. Kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na umaskini, ujinga na maradhi, mwaliko kwa wananchi wa Canada kusali na kuwaombea, lakini zaidi kuonesha mshikamano wao wa upendo kwa hali na mali.

Katika Njia ya Imani, Maaskofu wanakiri kwamba, haki, amani na maridhiano kati ya watu yametoweka na matokeo yake: Vita, chuki na uhasama vinatawala katika mioyo ya watu. Kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea kumwagika huko Mashariki ya kati, lakini Jumuiya ya Kimataifa bado haijasikiliza kwa makini na kujibu kwa uhakika kilio hiki cha damu. Wakristo wanaendelea kunyanyaswa, kudhulumiwa na hata kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kuna watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa sababu ya imani; wote hawa wanapaswa kusindikizwa na kusaidiwa kwa hali na mali. Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni wajenzi wa amani na wajumbe wa matumaini mapya kati ya watu. Viongozi wa Serikali, Jumuiya ya Kimataifa pamoja na wadau mbali mbali wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kusimamia haki msingi za binadamu. Wawe mstari wa mbele kutafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi; huku utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika tafakari ya Vituo vya Njia ya Msalaba, kila kituo wameweka nchi moja ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekumbana na majanga mbali mbali. Kwa mfano Ufilippini ambayo kwa mwaka 2013 ilitikiswa na tufani ya Hayani iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali. Maaskofu wanaombea mchakato wa haki na usawa katika masuala ya biashara ya kimataifa huko Colombia. Kuna maelfu ya wananchi ambao ni maskini wamepokonywa ardhi yao ambayo kwa sasa inatumika kuzalisha nishati uoto.

Maaskofu wanaendelea kuwakumbuka na kuwaombea watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaofariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Wanawakumbuka watu ambao wanaendelea kuogelea katika umaskini wa hali na kipato kutokana na sera na mifumo duni ya maendeleo. Maaskofu wa Canada katika Njia ya Mshikamano wanawapongeza wakulima nchini Brazil ambao wameanzisha Benki ya Wakulima ili kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo wa uzalishaji kwa kusaidiana kupata mbegu bora na pembejeo za kilimo kwa bei nafuu.

Maaskofu Katoliki Canada katika tafakari yao ya Ijumaa kuu, wanazingatia pia umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho, kwa kusaidia mchakato wa kilimo bora kama vile Ethiopia, Zambia na Cambodia. Wanawakumbuka wananchi wa Sierra Leone ambao kwa miezi kadhaa wameteseka na kutikiswa sana kutokana na janga la ugonjwa wa Ebola. Wote hawa wanakumbukwa katika sala na tafakari, ili kweli Wasamaria wema waendelee kusaidia mchakato wa kutafuta kinga na tiba ili kutokomeza ugonjwa wa Ebola ambao umekuwa ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya wananchi wengi Afrika Magharibi.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kulinda na kutunza mazingira, kwa kufanya mabadiliko ya kweli katika mtindo wa maisha, kwa kuwaheshimu wengine pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.