2015-04-02 09:48:00

Maisha, dhamana na wito wa Mapadre


Majiundo makini ya Wakleri na mabadiliko msingi ndani ya Kanisa ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Familia yote ya Mungu; lakini Askofu mahalia na Mapadre wakiwa mstari wa mbele. Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linayowaandikia Mapadre wake, barua ambayo inamguso wa kifamilia.

Maaskofu wanawashukuru Mapadre kwa kwa moyo wa dhati kutokana na sadaka na majitoleo yao yanayoonesha ushuhuda wa imani tendaji kwa kuwahudumia: wanaparokia wao, kuwafunda na kuwafundisha vijana na watoto; kusindikiza familia katika maisha na utume wake; kwa kuwatembelea na kuwahudumia wagonjwa pamoja na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Maaskofu wanawakumbuka na kuwaombea Mapadre wagonjwa, wazee na wale wanaokabiliana na kinzani katika maisha na utume wao wa Kipadre.

Barua hii inapata chimbuko lake kutokana na majadiliano ya kina na mapana wakati wa maadhimisho ya mkutano wa 67 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, waliokuwa wanakutana mjini Assis, hivi karibuni. Maaskofu wamepembua kwa kina na mapana kuhusu maisha na majiundo ya kudumu ya Mapadre, kwani haya ni mambo ambayo wanapenda kuyapatia kipaumbele cha pekee mintarafu mwelekeo unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kulipyaisha Kanisa, kwa kuanzia kwanza katika maisha ya Mihilimi ya Uinjilishaji.

Wakati huu, utume wa Mama Kanisa na maisha ya Jumuiya za Kikristo hayana budi kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii kwa wakati huu, na pale Mapadre wanapohusika, wanachafua utume na maisha ya Mama Kanisa. Maaskofu wanawashukuru Mapadre kwa kazi njema wanazotenda katika maisha na utume wao, lakini wanasema kuna haja ya kuboresha maisha na wito wa Upadre, ili magumu na changamoto za maisha, kamwe zisizimishe ile furaha, ari na moyo wa kimissionari; daima wakiwa makini katika mang’amuzi yao, huku wakiongozwa na sala na majitoleo kwa wote wanaohitaji msaada wao; unaofariji na kuhekimisha ikiwa kama, Mapadre hao wanaishi kadiri utashi wa Mungu.

Maaskofu wanasema, majiundo makini na mchakato wa mabadiliko ndani ya Kanisa ni mambo yanayoigusa Jumuiya yote ya waamini na kwamba, Upadre unakuwa ni mahali ambapo watu wanakutana ili kushirikishana ile karama ya ubaba na udugu; mang’amuzi na msaada kwa wale wanaohitaji. Maaskofu wanatambua kwamba, mabadiliko makini ndani ya Kanisa yanaweza kufanywa na Mapadre kwa kukazia utambulisho wao wa Kikuhani.

Maaskofu wakiwa wameungana kwa pamoja katika kifungo cha mshikamano unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Daraja Takatifu, wanataka kuwahimiza Mapadre kuishi na kutenda kadiri ya moyo wa Mungu, huku wakijitahidi kuiga mfano na moyo wa Kristo mchungaji mwema. Upendo wa Kristo kwa Kanisa lake uwe ni kiini cha wito wao wa Kipadre katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali.

Wakleri wanatambua kwamba, wanabeba dhamana kubwa ya utume wao kwa Familia ya Mungu na kwamba, wanahisi kuwa ni mzigo mkubwa usioweza kubebeka na waamini kutokana na mapungufu na dhambi zao kama binadamu. Wanapenda kuwahudumia Watu wa Mungu kwa upendo mkamilifu, huku wakionesha unyenyekevu, makini na tayari kufanya toba na wongofu wa ndani. Hakuna mabadiliko ya kweli yanayoweza kufanywa kwa mtu, ikiwa kama mtu mwenyewe hatagundua kwamba, anahitaji kusaidiwa, kusahihishwa, kufundwa na kurekebishwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linahitimisha barua yao kwa Mapadre kwa kuwaombea katika maisha na wito wao, ili waweze kurekebisha mapungufu yao na hatimaye, utukufu wa Mungu uweze kung’aa tena, katika furaha na ubora wa maisha ya Kikristo; katika moyo wa upendo na udugu; kwa kushirikishana na kutaabikiana na watu wanaowahudumia; huku wakitambua kwamba, wanawapenda, wanataka kuwasaidia na kujisadaka na kwa vile wanatarajia pia kupata mengi kutoka kwa Mapadre. Furaha na wongofu wa ndani, katika mchakato wa kujitakatifuza, uwasaidie Mapadre kutambua ukuu wa wito na maisha ya Kipadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.