2015-04-02 15:21:00

Daraja takatifu ni Sakramenti ya huduma kwa Familia ya Mungu


Wapendwa wana ukoo wote na familia ya Mungu popote pale ilipo! Litukuzwe Fumbo la Ekaristi Takatifu! Napenda kuungana na wengine wana ukoo ambao tayari wamekwisha fanya hiki ninachotaka kukifanya nami: kuwatakieni nyote heri sana kwa siku ya leo ya "Alhamisi kuu", siku tunapoanza kuadhimisha siku zile tatu kuu za Fumbo letu la Ukombozi kupitia mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo!

Katika salamu ambazo wengi wametutumia sisi Mapadre wenu kupitia mtandao wa "whatsApp" au kama wasemavyo wengi "wasapu", tumepewa salamu za heri ya siku ya leo, hasa wamepelekewa salamu hizi mapadre, ambao kwa maelezo ni kwamba siku ya leo, miaka zaidi ya 2000 ilopita Bwana wetu Yesu kristo aliweka sakramenti ya daraja takatifu. Kwa maana nyingine siku hii ya leo tunakumbuka siku ile mapadre tulipoandaliwa "ajira"! Asante Yesu! Pamoja na salamu hizo na heri hizo, nami nimependa basi kwanza niwashukuruni nyote mliotutakia heri hizo, pili niwatakieni pia ninyi makasisi wenzangu pia heri, neema na baraka tele kwa siku hii ya leo, na tatu niwashirisheni nyote dondoo zangu kwa siku hii ya leo.

Siku ya Alhamis kuu Bwana wetu Yesu Kristo akiwa katika ukamilifu wake, aliweka sakramenti ya daraja takatifu la Upadre, hilo alilifanya kwa maneno yale: alipotwaa mkate akawaelekea wanafunzi wake na kuwaambia huu ndio mwili wangu, na akatwaa kikombe akisema hiki ni kikombe cha damu yangu, damu ya agano jipya itayomwagika kwaajili ya wote, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Ndivyo anavyotuandikia mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa wakorintho.

na baada ya kufanya hilo akajifunga "kibwebwe" akachukua beseni lenye maji na kuanza kuwaosha miguu yao. Kuosha miguu ili kuwasafisha kimwili, lakini yeye hasa alichotaka hapo ni kuweka alama ya kusafisha kiroho, maana yake hao aliowapokea na kuungana nao kwa kuwapa mwili wake wale, yaani wawe ndani yake na yeye ndani yao, bado anaona kuna hitaji la kuwatakasa kabisa ili muunganiko huo naye uwe pia ni muunganiko wa kujitaka na kutakaswa.

Mtakumbuka wapendwa, katika tukio hilo la kuwaosha miguu alipofika kwa Simon Petro, huyu aliweka pingamizi. Simoni Petro ambaye kila mara tumekuwa tukimsikia akiwa na kimbelembele cha "kutumbukiza mguu wake" kwa kila jambo ambalo lilipasa utendaji fulani. (tujikumbushe alivyotoa upanda na kumfyeka sikio yule mtumishi wa maaskari siku wanakuja mkamata Yesu, tukumbuke alivyojibia juu ya Yesu ni nani, tukumbuke alivyomkanya Yesu juu ya kukubali kuteswa, nk) lakini sasa anakuwa wa kwanza "kutoa mguu wake" toka ndani ya beseni la kuoshwa.

 Simoni Petro hapa alielewa tu uoshaji wa kawaida, wa mwili na sio wa kutakaswa, ndio maana alipoambiwa kuwa ile ni ishara tu ya kuonyesha kuwa mmoja amepokelewa kuwa mwanashirika, ndio anaripuka na kusema, "Bwana si tu miguu bali mwili mzima" Bado simoni Petro anawaza juu juu hajaelewa juu ya alama. Kumbe, kwa kuwaosha miguu yao anawapa uthibitisho kuwa wametakaswa, wameondolewa dhambi zao, na hivi wamepokelewa katika ushirika na Bwana, na zaidi sana kwa kutumia alama hiyo ya kibinadamu, "maji" iliyo alama ya uhai na usafi, ndio anawaeleza na anatueleza sote, kuwa japo tumepokelewa, japo tu washirika lakini tukumbuke kuwa sisi ni binadamu, hivi tutaendelea kuchafuka, lakini tuna pa kujisafisha na tuna zana za kujisafishia, ndio maji. Kwa maneno mengine, anasema anawekea maji hayo yatuimarishe, yatupe nguvu za kusonga mbele katika umoja naye.

Maji kwa kuwa pia ni kiburudisho na ni faraja, basi pia kwa kuwaosha hao kwa kutumia maji, anatueleza kuwa pale tutapopata uchovu, tunapopata udhaifu, tutapoelekea kukata tamaa, tuinuke, tusafishane, tufarijiane tuimarishane, kwani sisi tu wamoja. Na hilo ndo analikamilisha pale anapowauliza, "je mmeelewa hilo?" "nanyi hudumianeni kwa mtindo huo! Ekaristi Takatifu, anaionyesha hapa kuwa kumbe ni huduma kwa jamii huduma sisi kwa sisi na hasa ni alama ya upendo wa kibinadamu, ni ubinadamu kupendana na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.

Kumbe ndugu zangu, ukifuatilia matendo hayo yote ya siku hiyo ya alhamisi kuu utagundua kuwa bwana wetu Yesu Kristo alihitimisha pia kuweka sakramenti zile zote saba. Nimejaribu ku-highlight hapo kwa wino mweusi mnene mambo ambayo nadhani yanaweza kutusaidia kuchambua zaidi juu ya hilo nilolieleza hapo mwishoni. Ukiyahesabu hayo utayakuta saba na nimeona yanaendana sana na zile sakramenti saba. Na hivi nikiungana na mababa wa mtaguso wa pili wa Vatican, waliotueleza katika ile hati juu ya Liturujia ya Kanisa “Sacrosanctum concilium kuwa Ekaristi Takatifu ndio kiini/chanjo na kilele cha maisha yote ya mkristo. (linganisha, Sc.10) ndio naweza kusema kuwa kwa kuwa leo ndio iliwekwa pia sakrament hiyo ya Ekaristi takatifu, basi leo pia ndio hata hizo Sakramenti nyingine zinapasa uhakika wake kuwa ziliwekwa naye, hata kama tunaelezwa matukio mbalimbali ya wakati mwingine ambapo ndio hizo sakrament nyingine ziliwekwa.

Basi ndugu zangu, nami mwenzenu nikiwa katika "unyonge na udhaifu" wangu, napenda kushirikiana nanyi na kuwashirikisha hayo, nikiomba sala zenu, lakini pia mawazo yenu katika tafakari ya siku hii ya leo, ya siku kuu hizi tatu zilizopo mbele yetu, na zaidi sana ya maisha yetu kama binadamu, kama wakristo na hivi kama ndugu wa familia moja.

Salaamu na heri kwenu nyote. Msichoke kuwakumbuka na kuwasindikiza Mapadre wenu kwa sala na sadaka zenu! Inapendeza mbele ya Mwenyezi Mungu.

Padre Tumaini Litereku Ngonyani

Jimbo kuu la Songea.








All the contents on this site are copyrighted ©.