2015-04-01 12:03:00

Juma kuu: Kumbatieni Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu!


Wakati huu Mama Kanisa anapotafakari kuhusu mafumbo makuu ya wokovu yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutetea Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu. Waamini wanakumbushwa kuchuchumilia upendo wa Mungu ambao una nguvu zaidi kuliko kifo na kwamba, wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao. Juma kuu na hatimaye, maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, iwe ni fursa ya kudumisha mahusiano mazuri katika medani mbali mbali za maisha.

Juma kuu ni wakati muafaka uliokubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa waamini kushuhudia upendo na matumaini kwa kuwasaidia wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali na kuwaonjesha matumaini wale wanaopambana uso kwa uso na kifo. Waamini wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, hawawageuzii jirani zao kisogo kama walivyofanya wale Askari kwa kuweka jiwe kubwa mlangoni pa Kaburi la Yesu, bali wawe ni cheche za imani, matumaini na mapendo kwa ndugu na jirani zao, ili watu waweze kuona mwanga na hatimaye, kushuhudia Injili ya Uhai.

Kutokana na utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia, waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaowaonjesha jirani zao upendo na kuwatia nguvu wale walioko kufani, ili kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa jamii husika sanjari na kuwaonjesha matumaini hata baada ya kifo.

Waamini waoneshe mshikamano wa upendo na udugu kwa watu wanaopambana na utamaduni wa kifo, watu wanaotaka kusimama kidete dhidi ya utumwa mamboleo, nyanyaso, dhuluma na umaskini. Wawe tayari kuwaunga mkono katika mapambano yote haya, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Waamini wawe na ujasiri wa kutambua na kukiri makosa na mapungufu yao, tayari kukimbilia wema na huruma ya Mungu na kwamba, watakatifu ni wadhambi waliotubu na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu.

Kumbe, kila mwamini anaweza kuwa kweli ni mtakatifu ikiwa kama atajibidisha na kutekeleza dhamana yake barabara. Waamini wasimame kidete kupinga nyanyaso na ukosefu wa misingi ya haki, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.