2015-03-31 08:52:00

Mwaka wa Watawa Duniani: Kongamano la malezi ya kitawa kutimua vumbi!


Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani unaoendelea kutimua vumbi sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 11 Aprili 2015 kunafanyika kongamano la kimataifa linalowashirikisha walezi katika maisha ya kitawa na kazi za kitume. Zaidi ya washiriki 1,200 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanashiriki katika kongamano, ili kuangalia fursa, matatizo na changamoto wanazo kabiliana nazo katika mchakato wa majiundo ya watawa wa leo na kesho. Mada hamsini zitachambuliwa kwa kina na mapana, ili kuweza kukabiliana na changamoto za malezi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kongamano hili linawashirikisha pia wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri pamoja na Baraza la kipapa kwa ajili ya elimu Katoliki. Kongamano la malezi ya kitawa litafunguliwa kwa mkesha unaoishirikisha familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Gregory wa VII hapo tarehe 7 Aprili 2015.

Jumamosi tarehe 11 Aprili, majira ya asubuhi, Kardinali Braz di Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya hitimisho la kongamano la malezi ya kitawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.