2015-03-30 14:54:00

Huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini!


Siku ya Alhamisi kuu, Mama Kanisa anakumbuka kwa namna ya pekee Siku ile iliyotanguliwa kuteswa kwake Yesu, akaweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu la Upadre na kielelezo cha huduma ya upendo kwa kuwaosha wanafunzi wake miguu, ili waweze kujifunza kutoka kwake. Alhamisi kuu ni Siku kuu yenye utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu, tarehe 2 Aprili 2015 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho katika Gereza kuu la Rebibbia lililoko hapa mjini Roma, kuanzia majira ya 11:30 jioni. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu atawaosha miguu wafungwa kama kielelezo cha huduma ya upendo hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huu ni mwendelezo wa utamaduni ambao Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, miaka miwili iliyopita amekuwa akiupatia kipaumbele cha kwanza. Itakumbukwa kwamba kunako mwaka 2013 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Gereza la Watoto watukutu la Casal del Marmo na mwaka 2014 ameadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu miongoni mwa walemavu wanaohudumiwa na Mfuko wa Padre Gnocchi.

Padre Sandro Spriano, mhudumu wa maisha ya kiroho Gereza kuu la Rebibbia anasema, Baba Mtakatifu ameitikia mwaliko wao kwa kuonesha mshikamano wa pekee kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa wakati huu wafungwa ambao wanakabliana na hali ngumu ya maisha kutokana na magereza mengi nchini Italia kufurika kiasi cha kutisha. Kwa mara ya kwanza, wafungwa wa kike na kiume wataungana pamoja kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Sandro Spriano anabainisha kwamba, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko gerezani pale una lengo la kuwaimarisha ndugu zake katika imani na matumaini ya kuweza kuwa watu bora zaidi wanapohitimisha adhabu yao na kumbe, hii ni hija ya kichungaji. Gerezani pasiwe ni mahali pa kulipiziana kisasi, bali mahali pa mkosaji kufundwa upya, ili aweze kurejea na kuendelea tena na maisha yake kwa matumaini makubwa zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.