2015-03-30 11:16:00

Hii iwe ni fursa ya kuufunda moyo kwa kukimbilia huruma ya Mungu!


Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu kwa upendo mkuu, akampatia wajibu wa kuendeleza kazi ya uumbaji, lakini baadaye alipoyaangalia matendo ya mwanadamu, akasikitika sana na kujiuliza kwa nini alikuwa amemuumba mwanadamu. Mwenyezi Mungu alikuwa anaangalia kile kilichokuwa kimefichika moyoni mwa mwanadamu, akashindwa kuona alama ya upendo na ile sura ya upendo wa moyo wake.

Matukio mbali mbali yanayoendelea kupamba kurasa za magazeti na picha za televisheni kwa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na vitendo vya kigaidi; wahamiaji kuzama na kufa maji kwenye tumbo la Bahari ya Mediterannia; maelfu ya  watu wanaofariki dunia kutokana na majanga asilia, vita na njaa, dhuluma na nyanyaso za kidini, kiasi hata cha kuibua makundi ya wafiadini sehemu mbali mbali za dunia.

Hapa kwa hakika anasema Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo la Kijeshi Italia katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2015, Mungu anashindwa kumwangalia mtu yule aliyemuumba kwa upendo wa moyo wake. Dhambi ilipozidi duniani, mwanadamu akakengeuka na kuiacha Sheria ya Mungu, akakiona cha mtema kuni kwa gharika iliyotokea wakati wa Nuhu, kwani watu walipewa nafasi ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, lakini mwaliko huo ukaonekana sawa na kumpigia mbuzi gitaa!

Kwaresima ya Mwaka huu, iwe ni fursa makini kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu hali ya maisha na mioyo yao, ili kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kuachana na mambo yale ambayo yanachafua moyo wa mwanadamu. Huruma ya Mungu bado ipo kama ilivyokuwa kwa Nuhu na familia yake waliookolewa kwa huruma na upendo wa Mungu, wakawa ni chachu ya imani, matumaini na mapendo; mwanzo mpya wa maisha ya mwanadamu.

Hija ya Kwaresima na hatimaye sherehe za Siku kuu ya Pasaka, iwe ni fursa ya kuunda moyo kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Inaonekana watu wameanza kuzoea kuona picha za mauaji ya kutisha na wala si tena sehemu ya habari inayotisha bali ni uhalisia wa maisha ya mwanadamu wa leo.

Hapa mwanadamu hana budi kuunda moyo wake kadiri ya mpango wa Mungu kwa kuguswa na shida na mahangaiko ya wengi, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kwaresima ni kipindi kigumu katika hija ya maisha ya kiroho, lakini ni muda uliokubalika wa kupambana kufa na kupona na mambo ambayo yanavuruga na kuvunja moyo; mambo yanayotishia na kuwakatisha watu tamaa na badala yake, Kwaresima kiwe ni kipindi cha kuimarisha imani, matumaini na mapendo. Ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani, muda wa kukua na kuimarika kwa kutambua kwamba, wamekombolewa kwa huruma na mapendo ya Mungu na wala si kwa mastahili yao binafsi. Upendo wa Mungu uwasaidie wale walioanguka kusimama tena kwa neema ya Sakramenti za Kanisa. Kwaresima ni kipindi cha kumwilisha upendo katika matendo ya huruma; kwa kuwaonjesha wengine ukarimu kwani mapendo ya kweli yanaunda moyo wa mwanadamu.

Kwaresima anasema Askofu mkuu Santo Marcianò ni kipindi cha kusali, kutafakari na kufunga, ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaokoa. Kwaresima iwe ni fursa ya kuunda moyo kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa mkuki, humo zikatoka Sakramenti za Kanisa. Waamini wasiwe wepesi kujiachilia mikomoni mwa Shetani ili awe ni dira na kiongozi wa maisha yao, hapa wanapaswa kupambana na Shetani pamoja na mambo yake yote hadi kieleweke!

Moyo uwe ni mahali pa kuamini, kupenda na kutumainia. Kwa njia ya mweleko huu, waamini wanaweza kusherehekea vyema Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.