2015-03-29 12:06:00

Wafunulieni watu upendo na huruma ya Mungu


Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa mahakama kuu ya kitume ya Kanisa Katoliki anabainisha kwamba, kwa mwamini ambaye ni mkweli, mwadilifu, mchamungu na mpenda haki na amani, kwa macho na mtazamo wa wengi katika ulimwengu huu wa utandawazi ataonekana kuwa kama amepitwa na wakati.

Kardinali Mamberti ameyasema hayo, hivi karibuni wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa wanachama wa Chama cha Mtakatifu Petro, baada ya kufanya Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma. Waamini wanakumbushwa kwamba, matendo mema na maadilifu ni matunda ya muungano wa kweli na Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani, inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Kuna maelfu ya watu wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia, lakini ni watu wenye imani, matumaini na mapendo thabiti; Mwenyezi Mungu atawakomboa kwa wakati muafaka. Uwepo wa Mungu kati ya watu wake ni ukweli ambao wakati mwingine watu hawapendi kuupokea na kuukumbatia kwani wanadhani kwamba, Mwenyezi Mungu ni kiwazo na kizingiti cha uhuru na maisha yao.

Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ndiye aliyewafuliwa binadamu ile sura, huruma na upendo wa Mungu unaokoa. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kushiriki maisha ya Mungu ambaye ni upendo, kwa kuwa kweli ni vyombo vya upendo kwa jirani zao. Kama sehemu ya maandalizi ya Juma kuu, Kardinali Mamberti kwa muda wa siku kadhaa amekuwa akitoa tafakari ya Neno la Mungu, ili kuwasaidia waamini kuguswa na huruma pamoja na upendo wa Mungu katika maisha yao pasi na kukata tamaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.