2015-03-29 12:29:00

Mchakato unaopania kudumisha amani duniani!


Mauaji, madhulumu na nyanyaso kwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto kubwa ambayo imetolewa na Patriaki Louis Raphael Sako wa Kanisa la Wababilonia Wakaldei, wakati alipokuwa anazungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kuna wazo linaloendelea kujitokeza katika Jumuiya ya Kimataifa kwamba, mauaji na dhuluma kwa Wakristo na makundi madogo madogo ya kiimani linapaswa kushughulikiwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa, kabla ya mambo hayaharibika zaidi. Kuna waamini wa dini mbali mbali wanaotaka kuishi kwa amani, maridhiano utulivu, lakini kuna baadhi wenye misimamo mikali ya kiimani, wanaotishia usalama na maisha ya jirani zao, kiasi hata cha kuhatarisha haki msingi za binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Patriaki Sako haina budi kulivalia njuga mashambulizi ya kigaidi, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kwa miaka mingi wameendelea kuonesha mshikamano wao wa dhati kwa Wakristo waliokuwa wanauwawa kinyama pamoja kudhulumiwa, lakini vitendo hivi havikupewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa.

Kwa mara ya kwanza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejadili mada hii kwa kina na mapana, kiasi cha kuanza kutangazwa hata na vyombo vya habari kimataifa, kana kwamba, hii ni habari mpya! Wakristo wanadhulumiwa sana huko Syria, Iraq na Nigeria. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anabainisha kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakomesha mauaji ya Wakristo huko Mashariki ya Kati pamoja na kuibua mbinu mkakati wa kuzuia misimamo mikali, mkakati ambao unatarajiwa kuzinduliwa mwezi Septemba.

Umoja wa Nchi za Kiarabu hauna budi pia kuchangia katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu hususan kwenye mataifa ya Kiarabu. Kwa upande wake Patriaki Sako anabainisha kwamba, elimu na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya katika masuala ya kisiasa na kitamaduni; haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu ni mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumo wa pekee ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Watoto wapewe fursa ya kwenda shule kwani ujinga na ufinyu wa mawazo, unapelekea vijana wengi kujikita wametumbukizwa kwenye mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Ukosefu wa fursa za ajira, ukata na maisha magumu hususan miongoni mwa vijana; umaskini na hali ngumu ya maisha ni kati ya mambo yanayochangia vijana wengi kujihusisha na uvunjifu wa sheria, haki na amani.

Katiba za nchi zihakikishe kwamba, ubaguzi wa rangi na dini unakomeshwa kwani huu pia ni uwanja ambao unapelekea baadhi ya wananchi kujisikia kuwa ni wa daraja la piliĀ  hata katika nchi zao wenyewe, kwa vile tu wa imani tofauti. Hata viongozi wa dini wanapaswa kuwa makini katika mahubiri na hotuba zao kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia hekima na busara na kamwe wasiwe ni chanzo cha chuki, utengano na kinzani ndani ya jamii zao husika.

Udini na ukabila ni mambo yaliyopitwa na wakati, lakini bado yanaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Elimu makini na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa. Watu na nchi ambazo zinafadhili vitendo vya kigaidi kwa hali na mali, washughulikiwe kikamilifu kwani vitendo vyao ni kinyume cha amani, kama ilivyo kwa wafanyabiashara wa silaha duniani.

Waamini wa dini ya Kiislam wenye misimamo mikali ya kidini, inawawia vigumu kuishi na waamini wa dini nyingine na matokeo yake, wamekuwa mstari wa mbele kuwanyanyasa, kuwadhulumu na pamoja na kupania kuwafuta kutoka katika historia na kumbu kumbu za watu kama hali inavyojionesha huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.