2015-03-29 11:35:00

Kard. Parolin: Changamoto ni kupatanisha tofauti katika kweli na haki!


Mwelekeo wa kimissionari ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa inayohitaji mshikamano na ushirikiano katika medani mbali mbali za maisha. Lengo ni kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa Wakristo wanaoteswa na kunyanyasika huko Mashariki ya Kati; kusaidia kugharimia majiundo makini ya vijana Barani Afrika, ambao wengi wao wameguswa na kutikiswa na vita, kinzani na migogoro ya kidini, kisiasa na kikabila pamoja na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya ujana ndani ya Kanisa.

Haya ni kati ya mambo makuu ambayo Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amezungumza na wawakilishi  30 wa Jukwaa la Vijana Kimataifa, FIAC kutoka: Argentina, Italia, Romania, Hispania, Burundi na Rwanda. Changamoto kubwa inayoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa ni upatanisho katika utofauti. Dhana hii isipopewa kipaumbele cha pekee, vita, kinzani na misigano itaendelea kujitokeza duniani.

Hii inatokana na ukweli kwamba, watu wanatofautiana: kiimani, kitamaduni, kisiasa na kidini; mambo ambayo yanatumiwa na baadhi ya watu kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani na utulivu.  Wakristo wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa upatanisho, mkazo uliotolewa kwa namna ya pekee na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Wakristo wawe ni chachu na vyombo vya uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda makini wenye mvuto na mashiko.

Wakristo wawe ni vyombo vya majadiliano yanayojikita katika ukweli, haki pamoja na kuheshimiana, bila kusahau kwamba, kama Wakristo wanapaswa kuwa ni watu wa huduma kwa jirani, chumvi na mwanga kwa wanaoutafuta. Makubaliano mbali mbali yanayofikiwa hana budi kuwa na msingi wake katika imani na utashi wa kutaka kuyatekeleza hayo waliyokubaliana. Wakristo waendelee kuwa ni vyombo vya umoja na mshikamano ndani ya Kanisa; kwa kuunganisha vyama mbali mbali vya kitume katika utekelezaji wa maisha na utume wa Kanisa, anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.