2015-03-29 11:23:00

Jiandaeni kwa: Siku ya Vijana Duniani na Mwaka wa Huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Jumapili ya Matawi ambayo pia ni Jumapili ya Mateso ya Bwana, amewataka vijana sehemu mbali mbali za dunia kuendeleza hija hii katika majimbo na mabara yao, hadi hapo Julai, 2016 watakapokutana Jimbo kuu la Cracovia, Poland, wakiongozwa na Mtakatifu Yohane Paulo II msimamizi wa maadhimisho ya Siku za Vijana.

Tema itakayoongoza maadhimisho haya ni “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo 5: 7. Tema hii inashibana sana na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, changamoto kwa vijana na waamini wote kuhakikisha kwamba, wanaguswa na huruma ya Mungu, ili kuweza kuieneza miongoni mwao.

Baba Mtakatifu amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema kumkimbilia Bikira Maria katika sala, ili aweze kuwasaidia kuliishi vyema Juma kuu. Bikira Maria alikuwepo na kushuhudia Yesu akiingia kwa shangwe mjini Yerusalemu, lakini moyo wake kama ulivyokuwa kwa Mwanaye mpendwa, ulikuwa tayari kwa sadaka. Waamini wanaalikwa kujifunza kutoka kwake ili kuwa waaminifu na kumfuasa Kristo katika njia yake, hata kama wakati mwingine hii inakuwa ni Njia ya Msalaba.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea abiria 150 waliofariki dunia kutokana na ajali ya ndege ya Germanwings, hivi karibuni huko Ufaransa kwa kutambua kwamba, kati yao kulikuwemo pia wanafunzi kutoka Ujerumani. Watu wengi wameguswa sana na msiba huu na bado wanasubiri kufahamu ukweli wa mambo kwani hadi sasa habari zinazoendelea kusikika kutoka kwenye vyombo vya habari zinasikitisha sana! Baba Mtakatifu amewatakia waamini wote kheri na baraka kwa juma kuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.