2015-03-29 11:57:00

Acheni imani za kishirikina kwa mauaji ya walemavu wa ngozi!


Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linaishauri Serikali kwa kushirikiana na wananchi, inawasaka na kuwatia mbarani wale wote wanaojihusisha na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini humo; mauaji yanayofanywa kwa misingi ya imani za kishirikina, kwa kudhani kwamba, viungo vya walemavu wa ngozi vinaleta bahati, afya na kinga ya ugonjwa wa Ukimwi; mambo ambayo hayana ukweli wana msingi wowote, huu ni utamaduni wa kifo.

Ni vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba walemavu wa ngozi wanapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuthaminiwa kama wananchi wengine wowote nchini Malawi. Inasikitisha kuona kwamba, hata katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, bado watu wanaendelea kukumbatia imani za kishirikina kama njia ya kupata utajiri wa haraka, kinga na madaraka.

Tume ya haki na amani Malawi inasema umaskini hauwezi kuwa ni kisingizio cha kufanya dhuluma na nyanyaso kwa watu wengine, bali mafanikio ya maisha yanapatikana kwa kufanya kazi halali, kwa juhudi, akili na maarifa. Kuna haja kwa Jamii kushirikiana kwa karibu zaidi na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kwamba, walemavu wa ngozi wanalindwa na kuheshimiwa. Wanapaswa kujisikia kuwa ni watu huru katika nchi yao.

Ubora wa jamii kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, unapimwa kwa kuiangalia jamii jinsi inavyowahudumia wanyonge ndani ya jamii husika. Hakuna mahusiano yoyote kati ya viungo vya walemavu wa ngozi na masuala ya utajiri, kinga na madaraka! Wahusika wa vitendo hivi wakamatwe na wafikishwe mbele ya sheria kujibu mashitaka yatakayokuwa yanawakabili.

Vyombo vya sheria navyo vinapaswa kutenda haki na kukataa utamaduni wa kupokea rushwa ili kuwalinda wahusika. Utawala bora na utii wa sheria; utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na mafao ya wengi ni mambo msingi katika ustawi na maendeleo ya wengi. Viongozi wa kidini, Serikali na kisiasa hawana budi kusimama kidete kupinga mauaji ya walemavu wa ngozi, kwa kuwa na jamii inayojisimika katika misingi ya haki, amani na utulivu.

Watu wajenge na kudumisha utamaduni wa maisha, urithi kwa binadamu wote badala ya kutawaliwa na utamaduni wa kifo unaojikita katika dhana ya utajiri wa haraka haraka, kinga na madaraka. Mwanadamu ana utu, heshima na haki zake msingi na kwamba, maisha ni matakatifu kwani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.