2015-03-28 14:50:00

Patriaki Mar Dinkha IV alijisadaka kwa ajili ya umoja wa Wakristo!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa ya msiba wa Patriaki Mar Dinkha IV wa Kanisa la Syria ya Mashariki na anapenda kuchukua nafasi hii kuitumia Familia ya Mungu nchini Syria salam zake za rambi rambi kutokana na msiba huu mzito. Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Mheshimiwa sana Patriaki Mar Aprem wa Kanisa Syria ya Mashariki anasema kwamba, Wakristo wamempoteza kiongozi mashuhuri, jasiri na mwenye hekima aliyewahudumia watu wake katika nyakati ngumu zilizokuwa na changamoto nyingi.

Marehemu Patriaki Mar Dhinkha IV aliteseka na kusononeka sana kutokana na mateso na mahangaiko ya wananchi huko Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee kabisa madhulumu ya Wakristo nchini Iraq na Syria, kiasi cha kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuangalia hatima ya maisha ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Haya ni mambo ambayo Baba Mtakatifu anasema walizungumza kwa kina na mapana alipomtembelea mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na majitoleo makuu yaliyooneshwa na Hayati Patriaki Mar Dhinkha IV katika mchakato wa maboresho wa mahusiano kati ya Wakristo, lakini kwa namna ya pekee kati ya Kanisa lake na Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu anamwombea amani na pumziko la milele na kwamba huduma yake iliyotukuka kwa Kanisa iwe ni changamoyo kwa Wakristo wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.