2015-03-28 08:52:00

Papa kukutana na Rais wa Italia 18 Aprili na Rais Obama 23 Sept. 2015


Kwa mara ya kwanza, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Sergio Mattarella wa Italia mjini Vatican, Jumamosi tarehe 18 Aprili 2015, majira ya saa 4: 00 za asubuhi kwa saa za Ulaya. Baadaye, Rais Mattarella atapata fursa ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Barack Obama wa Marekani, tarehe 23 Septemba 2015 wakati wa hija yake ya kitume nchini Marekani. Huu utakuwa ni mwendelezo wa majadiliano yaliyofanywa na viongozi hawa wawili wakati, Rais Obama alipomtembelea Baba Mtakatifu Francisko kunako mwezi Machi 2014.

Katika mazungumzo yao kwa wakati huo, waligusia masuala mbali mbali ikiwemo changamoto ya umaskini na umuhimu wa kuwahudumia wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; fursa za uchumi kwa ajili ya mafao ya wengi; ulinzi na utunzaji bora wa mazingira; haki na uhuru wa kuabudu; wakimbizi na changamoto zake.

Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani inabainisha kwamba, Rais Barack Obama anapenda kuendeleza mazungumzo haya wakati atakapokutana na Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kwanza nchini Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.