2015-03-28 11:44:00

Mt. Theresa wa Avila alikazia: Sala, Uinjilishaji na Maisha ya Jumuiya


Tarehe 28 Machi 2015, Kanisa linaadhimisha Jubilee ya Miaka 500 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa, sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Ni mtakatifu anayeng’aa na mfano wenye mvuto na mashiko kwa wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Ni muasisi aliyethubutu kuanzisha jumuiya za kwanza za Shirika la Wakarmeli.

Ni mtawa aliyebahatika kupata mang’amuzi ya kukutana na Yesu Kristo katika maisha yake, akawa kweli ni kielelezo cha maisha ya kuwekwa wakfu; sala na majadiliano endelevu kati ya Mungu na mwanadamu, katika maisha ya kijumuiya yanayofumbatwa ndani ya Mama Kanisa. Ni mwalimu wa sala, mtangazaji na shuhuda amini wa Injili ya Kristo aliyejitahidi kuimwilisha katika maisha ya kijumuiya.

Haya ni mambo msingi ambayo yameandikwa kwenye barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Padre Saverio Cannistrà, Mkuu wa Shirika la Wakarmeli wakati huu wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 500 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila.

Alikuwa ni mtu wa sala na mang’amuzi ya ndani aliyopenda kuwashirikisha wengine ili kujiunga katika mchakato wa majadiliano ya ndani na Kristo; majadiliano yaliyopamba maisha yake yote kwani alitambua kwamba alikuwa ni dhaifu katika sala, kumbe atambua umuhimu wa kuwa mdumifu katika sala licha ya shida, magumu na changamoto za maisha. Kama sehumu ya urithi wa maisha ya kiroho, wakati huu Kanisa linaoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, Mtakatifu Theresa wa Avila anawataka watawa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Yesu, mwalimu mahiri katika shule ya upendo kwa Mungu na jirani.

Mtakatifu Theresa wa Avila baada ya kukutana na Yesu katika maisha yake, akajaliwa kupata mageuzi ya ndani na kuanza kuwa kweli ni shuhuda na mtangazaji wa Injili ya Kristo kadiri ya mazingira na hali yake. Akajikita katika kumwilisha mashauri ya Injili  na kuanza mchakato wa mageuzi makubwa katika maisha yake binafsi na watawa wenzake. Aliwataka kuongeza bidii katika maisha ya sala kwa kuomba mambo msingi kwa ajili ya ulimwengu. Mwelekeo huu wa kimissionari na Kikanisa umekuwa ni utambulisho wa Wakarmeli duniani. Huu ni mwaliko wa kuuangalia ulimwengu kwa jicho la Kristo, ili kutafuta kile anachotafuta na kupenda.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kadiri ya utambuzi wa Mtakatifu Theresa wa Avila, sala na utume ni mambo msingi yaliyokuwa yanamwilishwa katika maisha ya kijumuiya yanayosimikwa katika msingi wa udugu na sadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani. Aliwataka watawa wenzake kujivika fadhila ya unyenyekevu na uchaji wa Mungu pasi na kujitakia makuu, chanzo cha majungu, wivu na misigano inayovunja mahusiano mema kati ya watu. Fadhila ya unyenyekevu, umissionari, kujikubali na kujiachilia mikomoni mwa Mungu ni chapa ya Mtakatifu Theresa.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya za Wakarmeli zinachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni nyumba za umoja, tayari kushuhudia upendo wa kidugu na umama wa Kanisa, kwa kumpeleka Kristo kwa wahitaji mbali mbali, sanjari na kuganga madonda ya migawanyiko na vita.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawashukuru Wakarmeli kwa kumweka chini ya tunza na ulinzi wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, kwa kuliombea Kanisa liweze kupambana na magumu na changamoto. Anawataka Wakarmeli kuwa mashuhuda kama alivyofanya Mtakatifu Theresa kwa kuwataka waoneshe furaha na uzuri wa kumwilisha Injili, chambo kwa vijana kujisadaka kwa ajili ya kumfuasa Kristo kwa karibu zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.