2015-03-28 09:30:00

Mikakati ya Kanisa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi nchini Nigeria!


Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linabainisha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi na wahamiaji millioni moja kutoka Nigeria ambao wamekuwa wakihudumiwa na Kanisa Katoliki ndani na nje ya Nigeria. Caritas Internationalis katika mkutano wake wa siku mbili uliohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Roma imejiwekea mbinu mkakati wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotaka kusalimisha maisha yao dhidi y a mashambulizi yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Mkutano huu umehudhuriwa pia na wajumbe kutoka Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Nigeria, Niger na Chad, wanaobainisha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi 800, 000 ambao wanahifadhiwa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Baadhi ya wakimbizi kutoka Nigeria wanahudumiwa pia huko Niger, Chad na Cameroon. Ni watu wanaoishi katika mazingira magumu. Mshikamano wa udugu na upendo kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon na Nigeria umeliwezesha Kanisa kuwahudumia wakimbizi wote hawa kwa kutambua na kuheshimu utu wao.

Wajumbe wanasema, kuna idadi kubwa ya wakimbizi wanaokimbia makazi yao ili kusalimisha maisha yao na kwamba, hii ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa huko Afrika Magharibi. Baada ya maboresho ya hali ya ulinzi na usalama, wananchi wengi wanaanza kuona cheche za matumaini Kaskazini mwa Nigeria. Maaskofu wa Nigeria wanakumbusha kwamba, si rahisi sana kuweza kukisambaratisha kikundi cha Boko Haram kutoka nje, hadi pale wahusika wakuu watakapobainishwa na kushughulikiwa barabara.

Boko Haram bado ni tishio kwa usalama na maisha ya wanchi wengi; kinaendelea kuteka nyara watu na kusababisha mashambulizi ya kushtukiza. Matukio haya yanaumiza na kukatisha tamaa. Boko Haram itaweza kusambaratishwa, ikiwa kama viongozi watakaoingia madarakani watakuwa na nia hii kwani kweli watu wamechoka kuendelea kukaa roho juu juu, kwa kuhofia usalama wa maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.