2015-03-28 12:14:00

Jumapili ya Matawi na maana yake!


Matawi ya Mizeituni yanayoupamba Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi tarehe 29 Machi 2015, yametolewa na Jimbo Katoliki la Cerignola-Ascli Satriano, lililoko Puglia, Kusini mwa Italia. Kazi hii ya sanaa imefanikishwa kutokana na mshikamano na umoja uliooneshwa na wadau mbali mbali, ambao kwa miaka 15 iliyopita wamekuwa wakitekeleza dhamana hii.

Askofu Felice di Molfetta anasema, Mama Kanisa anakianza Kipindi cha Juma kuu kwa Yesu kuingia Yerusalemu kwa shangwe. Hii ni shangwe ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii waliomtambua na kumwona Yesu kuwa ni Mwalimu maskini na mnyenyekevu, anayekuja kuwakirimia huruma ya Mungu na amani. Anapanda Punda bila ya kuwa na ulinzi wowote, anaongozwa na upendo ili kuonesha umuhimu wa majadiliano na mshikamano katika ukweli na haki na wala si kwa upanga na risasi.

Miti ya Mizeituni na mitende ni alama ya matumaini na amani, changamoto kwa waamini kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya amani katika medani mbali mbali za maisha. Matawi ya mitende yaliyobarikiwa ni alama ya imani kwa Mungu wa amani na maendeleo. Mti wa Mizeituni ni alama ya ibada na amani; furaha na faraja na kwamba, mafuta yake yanaupamba uso wa mwanadamu na kuondoa makunyanzi yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.