2015-03-28 09:23:00

Boko Haram bado ni tishio nchini Nigeria


Mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria ni kati ya changamoto kubwa zinazotakiwa kuvaliwa njuga na viongozi watakaoibuka kidedea katika uchaguzi mkuu unaofanyika nchini Nigeria, tarehe 28 Machi 2015. Katika kipindi cha miaka mitano, Boko Haram imesababisha majanga makubwa katika maisha, mali na miundo mbinu nchini Nigeria.

Watu wanaendelea kuishi kwa hofu na wasi wasi wa kushambuliwa wakati wowote, kiasi cha wananchi kuona kwamba, Serikali yao haina tena nguvu ya kuwahakikishia raia wake amani na usalama, mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu. Mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi ni agenda ambayo inapaswa kufanyiwa kazi mara moja mara tu viongozi wapya watakapopata ridhaa ya kuongoza wananchi wa Nigeria, vinginevyo, mustakabali wa Nigeria kwa siku za usoni, bado utaendelea kuwa mashakani.

Wachunguzi wa mambo ya kimataifa wanabaini kwamba, rushwa, ufisadi, tamaa ya mali na madaraka pamoja na udini ni mambo ambayo yamechangia kuporomosha demokrasia, utawala bora, utu na heshima ya wananchi wengi wa Nigeria. Boko Haram imekuwa ni chanzo kikubwa cha utengano na misigano ya kidini nchini Nigeria, jambo hili lisipoangaliwa kwa umakini mkubwa, Nigeria itaendelea kuogelea katika umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Bara la Afrika lina matumaini kwamba, kwa njia ya ushirikiano na mshikamano unaopania mafao ya wengi, Boko Haram inaweza kushikishwa adabu kama ilivyojionesha hivi karibuni vikosi vya ulinzi na usalama kutoka: Benin, Cameroon, Chad na Niger. Nigeria inahitaji kuboresha miundo mbinu yake, ili kuweza kukidhi mchakato wa mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni yanayoendelea kwa sasa. Ili kufikia lengo hili, kuna haya ya Serikali kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi unatumika kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa mtindo wa sasa ambapo kuna mamillioni ya wananchi wa Nigeria wanaoendelea kutumbukia katika baa la umaskini wa hali na kipato, wakati ambapo kuna kundi dogo la Wanigeria waliokula kuku kwa mrija!

Amani, usalama, utulivu na maridhiano na mambo msingi wakati n amara baada ya uchaguzi mkuu, kwani hizi ni nyakati ambazo nchi nyingi Barani Afrika zimejikuta zikitumbukia katika machafuko ya kisiasa na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Ikumbukwe kwamba, katika mashindano, kuna kushinda na kushindwa, wale wanashinda wakubali matokeo kwa heshima ya wananchi wanaowapatia ridhaa ya kuongoza nchi, wale wanaoshindwa, wajipange vyema kwa kuendelea kutafuta mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.