2015-03-27 08:01:00

Ukraine: Zingatieni kanuni na sheria za kimataifa!


Vatican inapenda kuwahakikishia wananchi wa Ukraine uwepo na mshikamano wake wa karibu hasa wakati huu wanapokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita inayoendelea nchini humo na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna haja ya pande zote zinazohusika kujikita katika sheria na kanuni za kimataifa kuhusiana na mipaka ya Ukraine, jambo muhimu sana ili kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa na pande zote zinazohusika.

Ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss wakati alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Alhamisi, 26 Machi 2015. Vatican inaridhia makubaliano yaliyofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuzitaka pande zote mbili kuhakikisha kwamba, zinasitisha mashambulizi na badala yake zinajielekeza zaidi katika majadiliano sanjari na kutekeleza makubaliano hayo kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Ukraine.

Vatican inatambua juhudi zilizokwishafanywa na Umoja wa Mataifa, OSCE na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla wake kama ilivyokubaliwa huko Minsk. Kuna haja ya kuendelea kuboresha hali na haki msingi za kibinadamu kwa kusitisha mapigano yanayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Mchakato huu unapaswa kusaidia kuachiliwa huru kwa wafungwa na mateka wote pamoja na kuhakikisha kwamba, nafasi inatolewa kwa ajili ya kutoa huruma ya kibinadamu.

Vatican inaonesha wasi wasi mkubwa kutokana na adha kubwa inayoendelea kujitokeza nchini Ukraine kwa watu wengi kuendelea kuwa maskini, kukabiliwa na baa la njaa na ukosefu wa usalama wa maisha na mali zao; mambo yanayochangia ukosefu wa huduma makini za afya kwa wananchi wengi. Kanisa Katoliki litaendelea kuchangia katika mchakato wa maboresho ya Ukraine kwa kupitia taasisi zake za huduma za kijamii na kwamba, Vatican ina imani na matumaini ya mshikamano wa upendo kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, ili kuwasaidia wananchi wa Ukraine kuanza tena mchakato wa maendeleo endelevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.