2015-03-27 10:14:00

Mshikamano wa upendo na udugu kwa Wakristo Iraq!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa karibu sana mateso na mahangaiko ya Wakristo na waamini wa dini nyingine nchini Iraq ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, nyanyaso na dhaluma, kiasi hata cha kuwa ni wakimbizi katika nchi yao wenyewe. Baba Mtakatifu anawakumbuka katika sala na sadaka yake na anatumaini kuwa wananchi hawa wataweza kurudi tena katika maeneo yao na kuendelea kuishi katika ardhi yao kama kawaida, huku wakiishi kwa amani na maridhiano na wote.

Familia hizi wakati wa maadhimisho ya Juma kuu, zinashiriki kwa namna ya pekee mateso yasiyokuwa na haki ya Yesu Kristo mwenyewe. Ili kuweza kuwa karibu na familia hizi, kwa mara ya pili Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu  anarudi tena nchini Iraq, ili kushiriki na Wakristo wa Iraq mateso ya Kristo, kwa kuonesha mshikamano wa Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Filoni Anawapelekea mchango uliotolewa na waamini wa Jimbo kuu la Roma, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na udugu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Baba Mtakatifu pia amechangia uwepo wake endelevu wa mshikamano kwa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Iraq.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.