2015-03-27 10:41:00

Maaskofu Pwani ya Pembe wakazia majiundo makini Seminarini


Umuhimu wa Seminari katika malezi na makuzi ya majandokasisi; majiundo makini na endelevu ya Wakleri sanjari na ufahamu wa kina wa Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ni kati ya mada kuu zilizochambuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, CECCI, wakati wa maadhimisho ya mkutano wake wa mia moja, tangu Baraza hili lilipoanzishwa. Mkutano huu umehitimishwa hivi karibuni huko Yamaussoukro, Pwani ya Pembe. Maaskofu katika tamko lao wanabainisha kwamba, wanapenda kukazia majiundo makini kwa majandokasisi tangu wakiwa kwenye hatua za awali pamoja na kuwaendeleza hatua kwa hatua, sanjari na kuwafunda pia walezi Seminarini ili waweze kutekeleza wajibu huu nyeti kwa hekima na busara.

Maaskofu wanatambua na kuthamini mchango unaotolewa na walezi katika Seminari mbali mbali nchini humo na kwamba, wanapaswa pia kukazia mwelekeo wa kimissionari kwa majandokasisi. Maaskofu wamewateuwa baadhi ya Majaalimu watakaosaidia kutoa majiundo makini kwa majandokasisi ili kupunguza uhaba wa walezi Seminari kuu. Maaskofu pia wamekutana na kuzungumza na ujumbe wa Umoja wa Mapadre Wazalendo, Pwani ya Pembe na kukazia umuhimu wa kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu kati ya Mapadre, ili waweze kutaabikiana na kusumbukiana wakati wa raha na shida.

Baraza la Maaskofu Katoliki limepembua kwa kina na mapana kuhusu changamoto za Mafundisho tanzu ya Kanisa; hali ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki; ukata mkubwa uliojitokeza baada ya Serikali ya Pwani ya Pembe kuondoa ruzuku pamoja na ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia na kuendesha shule hizi. Kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaohudumiwa kwenye madarasa kinyume cha kanuni za elimu pamoja na changamoto kutoka kwa walimu.

Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini humo; Kwaresima na hatimaye, maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka, kiwe ni kipindi cha upyaisho wa  maisha sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Waamini wanaendelea kuhamasishwa kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya haki, amani na upatanisho; kwa kuheshimu umoja katika tofauti kama alivyokazia Kardinali Jean Louis Tauran, alipotembelea nchini humo kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 110 ya Ukristo, nchini Pwani ya Pembe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.