2015-03-27 07:29:00

Hata maskini wana haki ya kutembelea Makumbusho ya Vatican!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 26 Machi 2015 amekutana na kuzungumza na watu 150 wasiokuwa na makazi maalum mjini Roma, kabla ya kutembelea Makumbusho ya Vatican na Kikanisa cha Sistina mahali ambapo Makardinali hukusanyika kwa ajili ya kusali, kutafakari na hatimaye kufanya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amesalimiana na watu hawa na kuwakumbusha kwamba, Kanisa ni nyumba ya wote na milango iko wazi kwa wale wanaotaka kukutana na Yesu Kristo. Hayo yamesemwa na Padre Ciro Benedettini, msemaji msaidizi wa Vatican.

Baba Mtakatifu amemshukuru Askofu mkuu Konrad Kraijewki, mtunza sadaka mkuu wa Papa kwa jitihada anazozifanya kwa ajili ya maskini na watu wasiokuwa na makazi mjini Roma. Baba Mtakatifu anasema, anahitaji sala na majitoleo ya watu kama wale katika maisha na utume wake. Amewabariki na kuwatakia imani na matumaini katika hija ya maisha yao, daima waonje huruma na upendo wa Kanisa. Watu hawa walipata chakula cha usiku na hatimaye kutembelea: Makumbusho ya Vatican, Kikanisa cha Sistina na Bustani za Vatican, maeneo maalum na kivutio kikuu cha watalii wanapotembelea Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.