2015-03-26 09:27:00

Simameni kidete kutetea utu na heshima ya binadamu!


Sala kwa ajili ya kuombea utume na maisha ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu pamoja na kuwakumbuka Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa huko Mashariki ya Kati, Asia na Afrika; ni kati ya mambo ambayo yamefanywa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati alipokuwa anahitimisha hija yake ya kichungaji nchini Hungaria, Jumatano tarehe 25 Machi 2015.

Ni jambo lisilokubalika baadhi ya waamini kuendelea kuuwawa kikatiliki kwa kisingizio cha misimamo mikali ya kidini na kuendelea kufumbiwa macho na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa.  Kuna Wakristo wanaonyanyaswa na kulazimishwa kuyakimbia makazi yao kutokana na chuki za kidini. Umefika wakati kwa wahusika kushughulikiwa kikamilifu kadiri ya sheria za kimataifa.

Kardinali Sandri ameyasema haya wakati wa maadhimisho ya Liturujia Takatifu kwa ajili ya kusherehekea Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu ni fursa kwa ajili ya waamini kukimbilia huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, Kanisa linaundwa na watakatifu pamoja na wenye dhambi.

Yesu Kristo analiwezesha Kanisa lake kuwa ni chemchemi ya neema, wema, uzuri na utakatifu wa maisha. Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu ni mwaliko wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kuokoa; changamoto ya kumwilisha imani katika matendo kwa kujikita katika mshikamano wa udugu na upendo.

Kardinali Sandri amemkumbuka kwa namna ya pekee, Mtakatifu Yohane Paulo II aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai kwa njia ya maneno na ushuhuda wa maisha yake. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukataa kishawishi cha kumezwa na malimwengu kwa kukumbatia utamaduni wa kifo, bali wasimame kidete kutetea utu na heshima ya binadamu; hasa miongoni mwa nchi changa duniani, ambazo zinageuzwa kuwa ni uwanja wa majaribio ya sera na utamaduni wa kifo. Hapa misaada ya kiuchumi na kijamii inafumbatwa katika masharti ya uzazi salama unaojikita katika sera za utoaji mimba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.