2015-03-26 10:08:00

Matajiri na maskini washirikiane kudhibiti athari za tabianchi!


Mataifa ambayo yanasababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kwa kuzalisha hewa ya ukaa yanayo dhamana ya kuchangia kwa kiasi kikubwa katika sera na mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao makuu mjini Genva, Uswiss alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa Tume ya haki msingi za binadamu ya Umoja wa Mataifa, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “ kukuza na kulinda haki msingi za binadamu; sanjari na haki ya maendeleo kwa kuheshimu mazingira.

Askofu mkuu Tomasi anabainisha kwamba, kuna mambo makuu matatu yanayopaswa kuzingatiwa, ili kupata haki jamii inayojikita katika usawa: kwanza kabisa ni mchango unaopaswa kutolewa na kila nchi kutokana na uwezo wake wa kiuchumi na kiwango cha maendeleo ya teknolojia; kwa kushirikisha teknolojia, ujuzi na maarifa katika uzalishaji wa malighafi pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka.

Mataifa ambayo yamefaidika kwa kiasi kikubwa na rasilimali ya dunia ina maana kwamba, yamechangia kwa kiwango kikubwa katika uzalishaji wa hewa ya ukaa, kumbe yanapaswa pia kuchangia zaidi, kama sehemu ya utekelezaji wa haki jamii. Ujumbe wa Vatican katika mada hii inayohusiana uchafuzi wa mazingira inakazia umuhimu wa kuzingatia pia haki msingi za binadamu.

Askofu mkuu Tomasi anawashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kuchangia katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu wanafanya mabadiliko katika mtindo na mfumo wa maisha ili kudhibiti athari za uharibifu wa mazingira zinazotokana na masuala ya kiuchumi na mazingira. Ni sehemu ya haki msingi na mshikamano wa kidugu kuwasaidia maskini na wote wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwani watu hawa hata pengine kwa kiasi kikubwa hawakuhusika na uchafuzi wa mazingira, lakini sasa wanateseka kutokana na athari zake.

Haki inaweza kutendeka kwa kuwasaidia wananchi wanaotoka katika Nchi changa zaidi duniani kupta teknolojia rafiki kwa mazingira, ili kupunguza kiwango cha uchafuzi wa mazingira. Macho ya Jumuiya ya Kimataifa yanaelekezwa zaidi nchini Ufaransa wakati wa mkutano wa athari za mabadiliko ya tabia nchi unaotarajiwa kufanyika mjini Paris, Mwezi Desemba, 2015.

Matajiri na maskini kwa pamoja wanaweza kuwa washindi, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itafanikiwa kufikia muafaka wa utekelezaji wa Protokali ya mwaka 2020 kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa. Nchi ambazo kwa sasa zinazalisha hewa ya ukaa kwa wingi zisaidie mchakato wa utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na mchakato wa udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.