2015-03-26 14:54:00

Jikiteni katika mchakato wa upatanisho, uponyaji na umoja wa kitaifa


Mchakato wa haki, amani na maendeleo endelevu ni kati ya mambo makuu ambayo Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni Dr. Olav Fykse Tveit na Bibi Ellen Margrethe Loj, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan ya Kusini wamejadili katika mkutano wao, uliofanyika hivi karibuni kwenye Makao makuu ya Umoja wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni mjini Geneva, Uswiss. Kwa pamoja wamepembua kwa kina mapana mambo ambayo yanaendelea kukwamisha mchakato wa upatikanaji wa amani ya kudumu nchini Sudan ya Kusini. Serikali ya wapinzani wanapaswa kutambua kwamba, haki na amani ni mambo msingi yanayohitajika ili kukoleza ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao kwa miaka mingi waliogelea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo lilikwamisha ustawi na maendeleo yao.

Makanisa nchini Sudan ya Kusini yanaendelea kukazia pia umuhimu wa amani Sudan ya Kusini na kwamba, juhudi hizi hazina budi kuungwa mkono na utekelezaji unaofanywa na viongozi wa Serikali na upinzani. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha kwamba, mchakato wa amani endelevu unapatikana Sudan ya Kusini. Sudan ya Kusini haina budi kujikita katika mchakato wa upatanisho, uponyaji na umoja wa kitaifa, ili kurejesha hali ya kuaminiana na kuthaminiana bila kutawala na uchu wa madaraka, upendeleo na ukabila mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa ni kikwazo katika mchakato wa amani ya kweli Sudan ya Kusini.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.


 








All the contents on this site are copyrighted ©.