2015-03-26 11:41:00

Furaha ya kweli inapata chimbuko lake katika imani


Imani na matumaini ya kukutana na Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ni chemchemi ya furaha ya kweli inayobubujikia maisha ya mwamini na wala si mafundisho butu! Ibrahim alionesha matumaini ya kuwa ni Baba wa Mataifa kwa kuzingatia ahadi aliyopewa na Mwenyezi Mungu, ingawa mke wake Sara alikuwa ni mzee na umri wa kupata mtoto ulikwishapita. Yesu aliwaambia walimu wa sheria kwamba, Ibrahim alitamani kuiona siku ya Mwana wa mtu na alipoiona alipata furaha kuu moyoni mwake. Walimu wa sheria hawakufahamu maana ya furaha ya Agano lililokuwa linafumbatwa katika matumaini. Ni watu waliokuwa wamepoteza dira na mwelekeo wa furaha, kwani furaha ya kweli inapata chimbuko lake katika imani.

Ibrahim, Baba wa imani, aliweza kufurahi kwa sababu maisha yake yote yalijikita katika imani, akawa ni mtu wa haki katika imani. Walimu wa sheria walikuwa ni mabingwa wa sheria lakini walikosa zawadi ya imani na kusahau kwamba, sheria inafumbata upendo kwa Mungu na jirani. Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, Alhamisi tarehe 26 Machi 2015 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martham, kilichoko mjini Vatican.

Walimu wa sheria walikuwa ni watu wenye imani haba, waliokuwa wanapindisha sheria na kuuliza maswali yenye mtego kwa Yesu. Ni watu waliopenda kuuona ulimwengu pasi na upendo, imani, matumaini na uwepo wa Mungu. Kwa mwelekeo huu wa maisha, anasema Baba Mtakatifu, hawakuweza kuwa na furaha mioyoni mwao, bali walishikwa na wasi wasi na kuwa na mioyo migumu. Inasikitisha kuona mwamini asiyekuwa na imani wala matumaini. Furaha inayobubujika kutoka katika imani na Injili ya Kristo ni jwe msingi la maisha ya mwamini, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia furaha inayojikita katika matumaini; neema ya kuona Siku ya Yesu, kwani Yeye ni chemchemi ya furaha ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.