2015-03-25 07:47:00

Watu 150 wamefariki kwa ajali ya Ndege, Ufaransa


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali ya ndege ya Germanwings, mali ya Kampuni ya Lufthansa, iliyoanguka nchini Ufaransa na kusababisha vifo vya watu 150 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo iliyokuwa inasafiri kutoka Barcelona kuelekea mjini Dùsseldorf. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Jean-Philippe Nault wa Jimbo Katoliki la Digne, Ufaransa, anapenda kutuma salam zake za rambi rambi kwa wale wote walioguswa na msiba huu mzito.

Anawaombea marehemu wote amani na huruma ya Mungu, ili aweze kuwapokea katika mwanga wa uzima wa milele. Anawaombea wale wote wanaojibidisha katika kazi ya uokoaji katika mazingira magumu. Baba Mtakatifu anawaombea faraja na kuwapatia baraka zake za kichungaji.

Viongozi mbali mbali wa Ufaransa, Ujerumani na Hispania wametuma salam zao za rambi rambi kwa familia zilizoguswa na msiba huu mkubwa. Uchunguzi wa chanzo cha ajali hii unaendelea kufanyika.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.