2015-03-25 14:38:00

Wanawake na utumwa mamboleo


Kila Mwaka tarehe 25 Machi, Umoja wa Mataifa unaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Waathirika wa Utumwa na biashara ya utumwa kupitia Bahari ya Atlantiki Siku hii hutoa nafasi kwa watu wote kuheshimu, kuomboleza na kuwakumbuka wale wote walioteseka na kufa chini ya mfumo katili wa utumwa. Siku hii inalenga kuhamasisha watu wafahamu na pia kushiriki katika kutokomeza aina zote za utumwa, ubaguzi wa rangi na dharau zinazojitokeza leo hii.


Kauli mbiu ya mwaka huu ni, “Wanawake na Utumwa”. Kauli mbiu hii inawaenzi wanawake wote watumwa waliovumilia mateso makali yakiwemo mateso ya kutumika vibaya kingono pamoja na kuwaenzi wanawake wote waliopigania uhuru kutoka utumwani na waliohakikisha utumwa unafutwa. Vilevile kauli mbiu hii inawasherehekea wanawake wote waliokuwa watumwa na ambao walifanikiwa kuwarithisha wanao jadi na tamaduni zao licha ya shinikizo mbalimbali na ukatili waliokuwa wakipitia.


Duniani kote kutakuwa na maadhimisho mbalimbali ikiwemo kusimikwa kwa ‘Sanduku la Mrejeo’ yaani Ark of return katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Hili Sanduku la mrejeo limetengenezwa na Rodney Leon ambaye ni msanifu wa Marekani kutoka Haiti. Ni chombo ambacho kimesimikwa kama kumbukumbu ya kutambua kuwa mamilioni ya watu wa Afrika walisafirishwa katika mazingira magumu. Wageni watapaswa kuingia katika sanduku la mrejeo ili kupata kwa undani uzoefu wa mambo matatu makubwa: kutambua uwepo wa janga hilo, kutafakatri kumbukumbu iliyobaki na kutosahau asilani.








All the contents on this site are copyrighted ©.