2015-03-25 15:02:00

Ukuu wa Punda!


Jumapili ya matawi: leo iko kazi kweli kweli: Marko 11: 1-10: Lengo ni huduma!

Mandhari ya fasuli ya leo ni ya Yeriko baada ya uponyaji wa kipofu Baltimayo, yasemwa: “Mara akapata kuona; akamfuata njiani,” yaani “kipofu kaona mwezi” mara moja anaamua kufuata msafara wa Yesu.  Mazingira haya yanaweza kufananishwa na ya mwanafunzi anayemwona Yesu na kuangazwa na matendo yake na mara kuamua kumfuata. Yesu alikuwa safarini akitokea Galilea kuelekea Yerusalemu-Yudea. Tunatajiwa mlolongo wa miji aliyopita Yesu, yaonekana miji hiyo ina maana yake, yaani, Yesu anapita Yeriko, Bethania Bethfage. Mji wa Bethfage ndiko alikoanza msafari wa kuingia Yerusalemu kwa shangwe akiwa juu ya punda au kihongo. Wakati Bethania upo umbali wa kilometa tatu tu toka Yerusalemu, mashariki ya mlima wa mizeituni. Toka huko mmoja unaweza kuiona vizuri Yerusalemu. Kuna pia barabara nzuri toka Bethfage hadi Yerusalemu. Hivi katika msafara wake akapitia Gethsemani hadi Yerusalemu na kuingia Hekaluni. Yasemwa pia kuwa siku ile alipopita alikuwa anachunguza mazingira ili asubuhi inayofuata aweze kupita na kuingia Hekaluni.

 

Yesu anawaagiza wanafunzi wawili na kuwaambia: “Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakalibili.” Hatujui ni kijiji gani kwani hakitajwi jina. Katika Biblia ukisikia kijiji kama unapata picha ya pahala ambapo watu wake wametulia, wanashikilia utamaduni, na hawako tayari kupokea mabadiliko na mambo mapya toka nje. Maisha ya kijijini yamepoa, ni tofauti na ya maisha ya mijini ambako kuna mchanganyiko wa watu, maisha yamechangamka na watu wamefunguka akili. Kumbe watu wa kijijini wamejifunga kidogo “hawajazibuka”, tena hawamwamini kirahisi mtu mgeni, watamwuliza maswali mengi.

 

Mfano mmojawapo wa watu wa kijiji unaona pale Yesu anapotaka kumponya mtu wa kjijini kwanza anamwitia nje ya kijiji. Baada ya kumponya anamwambia “usiingie tena kijijini,” kwa hoja kwamba akiingia kijijini atarudia hali yake ya upofu wa kuona mambo kwa ufinyu, yaani utashindwa kuona mwanga wa mambo. Kadhalika unaweza pia kuona katika maisha ya kawaida, watu wa kijijini wakiingia mjini wanazibuka akili hawapendi tena kurudi kijijini.

 

Yesu anaendelea kuwaambia wafuasi wake, “na katika kuingia ndani ya kijiji hicho, mara mtaona mwanapunda amefungwa, asiye pandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. Na mtu akiwaambia, ‘mbona mnafanya hivi?’ semini ‘Bwana ana haja naye, na mara atamrudisha tena hapa.” Punda huyo ananukuliwa hapa karibu mara nne ili kuonesha umaarufu na umaana wake. Huyo punda ndiye mhusika mkuu wa msafara wa Yesu. Katika Agano la kale mwanapunda anazungumziwa karibu mara mia moja na kumi na moja. Punda ni mnyama aliye ishara ya upole, unyofu, mchapakazi yaani alama ya utumishi. Tofauti na farasi anayejulikana kuwa ni mnyama wa vita na ni ishara ya uhodari, utawala, ufahari na ukuu. Punda na kondoo ni wanyama pekee waliochaguliwa kuonesha hali aliyo nayo Mungu.

 

Kitendo anachofanya Yesu cha kuingia Yesuralemu kwa shangwe akiwa juu ya punda, kinahitimisha unabii wa Zakaria anaposema: “Furahi ee binti Sioni.” Sioni ilikuwa sehemu ya watu fukara sana kwa vile ilikaliwa na watu waliotoka utumwani. Kadhalika unabii unasema, “Masiha amekaa juu ya punda na mafarasi na wapanda farasi wao watakimbia, naye mfalme aliye juu ya punda ndiye atakayewatawala,” yaani mfalme aliyepanda juu ya punda ndiye angeushinda na kuubadilisha ulimwengu kwa unyonge wake, tofauti na mategemeo yao.

 

Yatakiwa Punda huyo sasa afunguliwe, kwani bila kumfungua ufalme huo hauwezi kufika. Punda huyo alikuwa amefungwa kijijini, ishara ya watu wasiotaka mabadiliko. Aidha punda huyo alikuwa hajakaliwa bado na mtu yeyote yule mgongoni pake, kwa sababu watu wote wa wakati huo walikuwa wanapanda na kukaa juu ya farasi, alama ya ukuu, utawala, ufalme wa jadi, uonevu, ubabe, nk. Hii ndiyo picha ya ulimwengu wa kale unaotawala wanyonge. Sasa kumbe kuna mfalme mpya, mfalme wa amani, mpole, mnyenyekevu aliyejaa upendo.

 

Mwinjili anaonesha pia kwamba kuna watu wanaopinga kufunguliwa kwa huyo punda. Yesu alishalijua hilo kwa hiyo anaagiza, “mtu akiwaambia, mbona mnafanya hivi? ninyi mwambieni kuwa Bwana ana haja naye mara atamrudisha tena hapa.”

 

Mtu anayedadisi kufunguliwa kwa punda wala hata hakuwa mwenye punda, bali ni mwanakijiji tu fulani. Maana yake ni kwamba, kama punda ni alama ya utumishi, unyonge, unyenyekevu na farasi ni alama ya nguvu, utawala. Basi, punda ni nguvu ya upendo wa Mungu iliyo ndani mwetu inayotusukuma kumtumikia ndugu, kumhudumia, kumpenda na kumsaidia jirani. Lakini kuna pia nguvu ya farasi ndani mwetu inayotusukuma kutawala, kuonea, kukandamiza wengine ufahari nk. Kwa bahati mbaya nguvu ya unyofu, utumishi itokayo na upendo wa Mungu imefungwa ndani mwetu na inatakiwa kuifungua na ifanye kazi kwa uhuru. Ndiyo maana siyo mwenye punda anayeleta mizengwe ya kufunguliwa kwa punda huyo, kwani mwenye punda (hali hiyo ya kutumikia) aliye ndani mwetu ni Mungu mwenyewe. Kwa hiyo anayedadisi juu ya kufunguliwa punda huyo ni mwanakijiji, yaani walewale wasiotaka mabadiliko, wanakijiji, watu wafikra za kijadi wanaoshikilia fikra binafsi na wanaotaka kjijenga wenyewe tu na usimtumikie jirani. Kumbe Mungu anatuhitaji kumfungua huyo Punda. Ndiyo maana wafuasi wanamjibu wazi anayehoji kwamba “Bwana anamhitaji.”

 

Baada ya kuletwa mwanapunda, wafuasi “wakatandika migololi yao juu ya mgongo wa punda, naye Yesu akaketi juu yake.” Mgololi katika Biblia unamaanisha nafsi yaani mtu mwenyewe. Hata kwa mila za kibantu, mgololi ni mali ya mtu binafsi unaoonesha hadhi aliyo nayo mtu. Kutandika migololi juu ya punda na kukaliwa na Yesu, kunaonesha kujitoa kabisa nafsi yako na kuwa chini, kuupokea ufalme mpya anaoupendekeza Yesu. Punda anakuwa kiti cha enzi cha mfalme huyu mpya. Kumbe watu wengine “wakatandaza mavazo yao njiani na wengine matawi waliyoyakata mashambani.” Hiyo pia ni alama inayoeleweka katika Biblia, iliyoonesha kumshangilia na kumpokea mfalme wa Wayahudi anayeingia mjini juu ya farasi. Wanapaza sauti na kugumia “Hosana, ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; umebarikiwa na ufalme uzao wa baba yetu Daudi.

 

Hosana juu mbinguni.” Watu hao wanagumia kwa ushabiki kwa sababu wanafikiria na kuutazamia ufalme ule wa uzao wa Daudi, ule ambao unalingana na huu wa ulimwengu, ufalme wa mawazo ya kijijini. Watu hawa hawakuelewa yale aliyoyapendekeza Yesu, wanataka bado kuendelea utawala ule uliokuwa kabla ya kufika kwa Yesu. Ndiyo maana haiwezi kushangaza endapo watu hao hao ndiyo baadaye watamgumia, “asulibiwe”, kama vile wangesema: “Tulipitiwa, tulidhani huyu ndiye masiha, mfalme mpya, mwana wa Daudi.” Kwa hiyo hapa unaona kuna tawala za aina mbili, mosi ule wa utumishi (Punda) na pili ule wa ukuu (Farasi).

 

Yesu anaingia Yerusalemu baadaye anaenda Bethania. Baada ya kuona yote, siku ya pili asubuhi anafika kutimua watu hekaluni na ndivyo kutangaza ufalme wake mpya. Kuona maana ya upendo wa Mungu ulio katika mateso ya Yesu mwanae juu ya Msalaba ni sawa na kipofu Baltimayo aliyepata kuona. Nawe unaalikwa kama “Kipofu kaona mwezi” inuka na kumfuata Yesu njiani uishi na kuutangaza Msalaba ulio ishara ya hekima, huruma, upendo wa Mungu na ishara ya matumaini katika maisha. 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.