2015-03-25 08:59:00

Shuhudieni Injili ya Uhai na Injili ya Familia!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anabainisha kwamba, ili kweli Familia ya Mungu iweze kujikita katika kutangaza na kushuhudia utamaduni wa maisha, kuna haja ya kuwa ni watu wenye furaha, wanaowajibika na wakarimu. Mama Kanisa anaendelea kuwaalika watoto wake kufanya tafakari ya kina kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba 2015.

Kardinali Baldisseri ameyasema hayo, Jumanne, tarehe 24 Machi 2015 wakati alipokuwa anazungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia, kuhusu: wito na utume wa familia katika Kanisa na ulimwengu mamboleo, mada itakayochambuliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Tafakari hii inakwenda sanjari ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa Injili ya Uhai, akiitaka Familia ya Mungu kukumbatia Injili ya Uhai na kuachana na utamaduni wa kifo.

Kardinali Baldisseri anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake anaendelea kukazia umuhimu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaendelea kutishia uhai na usalama wa maisha ya mwanadamu, kwa kisingizio cha uhuru na haki msingi za binadamu; mambo yanayoungwa mkono na nguvu za kiuchumi, ubinafsi na uchoyo.

Kardinali Baldisseri anabainisha kwamba, haiwezekani kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kukumbatia utamaduni wa kifo unaopigiwa “debe” na sera pamoja na mikakati ya kiuchumi inayotafuta faida kubwa kwa gharama ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuhakikisha kwamba, kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuwaonjesha mshikamano na udugu unaosimikwa katika huduma.

Baba Mtakatifu Francisko anataka watu wakumbatie mwelekeo mpya wa maisha, kwa kufahamu Mafundisho tanzu ya Kanisa na kujitahidi kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha; kwa kuendelea kuwa waaminifu na wa kweli katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, tayari kuzimwilisha kama kielelezo cha imani tendaji.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, alikemea sana utamaduni wa kifo unaokumbatia: sera za utoaji mimba, vizuia mimba, kifo laini, uzalishaji kwa njia ya chupa, usawa wa kijinsia usiozingatia tofauti msingi kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na ndoa za watu wa jinsia moja. Yote haya ni mambo yanayokumbatia utamaduni wa kifo.

Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, kweli wanajikita katika utamaduni wa maisha, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai. Ikumbukwe kwamba, Injili ya Uhai ni chanda na pete na Injili ya Familia. Mafundisho ya Mwenyeheri Paulo VI kuhusu maisha ya mwanadamu na utakatifu wake, “Humanae vitae” bado ni muhimu sana katika mchakato unaopania kutukuza utakatifu wa maisha, ndoa na familia. Wakristo na watu wenye mapenzi mema, wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Uhai na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.