2015-03-25 09:47:00

Sala kwa ajili ya kuombea Sinodi ya Familia


Mama Kanisa tarehe 25 Machi anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, mwanzo wa Fumbo la Umwilisho, Siku ya Injili ya Uhai. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 25 Machi 2015 amejikita katika Sala kwa ajili ya Sinodi ya Familia kwa kuchambua Sala ya Bikira Maria pamoja na kusali na waamini waliokuwa wamefurika kwa wingi mjini Vatican ili kuhudhuria Katekesi yake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kujiandaa kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia anapenda kukazia kwamba, kuna uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Umwilisho na utume wa familia. Kadiri ya mpango wa Mungu, Yesu Kristo alizaliwa na kukulia katika familia ya binadamu iliyoundwa na Yosefu pamoja na Bikira Maria.

Kanisa linapoadhimisha Siku ya Uhai, linapenda kukazia umuhimu wa: maisha, utu na heshima ya kila binadamu. Tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu alipenda kuibariki familia na kuipatia dhamana ya kuendeleza kazi ya uumbaji; ili kweli iweze kuwa ni Jumuiya ya maisha na upendo katika moyo wa jamii. Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna uhusiano wa pekee kabisa kati ya Kanisa na Familia.

Mama Kanisa anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, anazisindikiza na kuziunga mkono familia, hasa zile zinazokabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali na kuombea Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, ili kweli Sinodi iweze kutafakari huruma ya Mchungaji mwema na hatimaye, kuliwezesha Kanisa kujikita zaidi na zaidi katika kushuhudia, ukweli na upendo wa Mungu kwa familia zote na kwamba, familia haina mbadala!

Familia ni kwa ajili ya mafao ya wengi, changamoto kwa waamini kukuza dhamana hii ndani ya: Familia, Kanisa na Jamii katika ujumla wake pamoja na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali kwa ari na moyo mkuu. Bikira Maria, Mama wa Mkombozi awe ni chemchemi ya furaha na faraja kwa wanafamilia wote. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wafanyakazi wengi ambao fursa zao za ajira ziko mashakani.

Ameitaka Jamii kuhakikisha kwamba, inatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshim ya binadamu; mshikamano na haki badala ya sera na uchumi unaojikita katika faida kubwa. Kazi ni kielelezo cha utu na heshima ya binadamu, lakini ukosefu wa ajira kisiwe ni kisingizio cha kujiingiza katika makundi maovu ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya Katekesi, alipitia kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI ili kukutana na kusalimiana na wagonjwa waliokuwa wanafuatlia Katekesi yake kwa njia ya Video. Amewakumbusha kwamba, Familia ya Mungu ni moja, inayokutana ili kusali, kutafakari Neno la Mungu, Katekesi na kushuhudia imani katika matendo. Amewaka wagonjwa kujiandaa vyema kwa Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa imani, matumaini na furaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.