2015-03-24 09:17:00

Wananchi wa Nigeria wamechoka, wanataka mabadiliko ya kweli!


Wananchi wa Nigeria wanatarajia kufanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 28 Machi 2015, lakini hali ya kisiasa na kijamii bado ni tete sana, kwani watu wanahofia usalama wa maisha na mali zao; umaskini wa hali na kipato unaendelea kuwanyanyasa wengi na kwamba, umoja na mshikamano wa kitaifa vinalega lega kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram.

Nigeria ni kati ya nchi tajiri sana Barani Afrika, lakini kutokana na vita, rushwa na kinzani za kidini na kijamii inajikuta inakabiliwa na changamoto nyingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake. Kardinali John Onayeikan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anabainisha kwamba, kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa siasa na demokrasia nchini Nigeria kwani watu wamechoka na ukosefu wa: haki na amani; demokrasia na maendeleo ya kweli.

Kiongozi yeyote yule atakayeshinda uchaguzi mkuu, ikiwa kama utafanyika, haba budi kuhakikisha kwamba, analeta mageuzi nchini Nigeria, ili kuwajengea tena wananchi imani katika utawala wa sheria, haki na amani. Wananchi wengi wamekuwa wakimbizi na wahamiaji katika nchi yao wenyewe, hawa wanataka mabadiliko ya kweli. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani, usalama, utulivu na mafanikio katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.