2015-03-24 10:05:00

Simameni kidete kutangaza Injili ya Uhai!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuihamasisha Familia ya Mungu nchini Perù kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Perù lina bainisha kwamba vitendo vya utoaji mimba si kielelezo cha maendeleo bali ni ukatili unaofumbatwa kwenye utamaduni wa kifo; maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu na wala si bidhaa inayozalishwa wala kutengenezwa kwenye maabara.

Maisha ni haki msingi ya binadamu na msingi wa haki nyingine zote, kumbe kuna haja kwa binadamu kuheshimiwa na kuthaminiwa katika hatua mbali mbali za ukuaji wake kwa kutambua kwamba, familia ni kitovu cha maendeleo ya mwanadamu. Familia haina budi kupewa kipaumbele cha pekee katika sera, dira na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa au na Serikali kwani familia ni kwa ajili ya mafao ya jamii nzima.

Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linaitaka Serikali kuheshimu zawadi ya uhai kwa kuondokana na utamaduni wa kifo unaokumbatiwa katika sera za utoaji mimba zinazotekelezwa Hospitalini kwa kisingizio cha uzazi salama. Utamaduni wa kifo unaendelea kuhatarisha maisha ya watu wengi kutokana na madhara yake. Jamii haina budi kutoa ulinzi na tunza kwa watoto ambao bado hawajazaliwa kwa kuondokana na utamaduni wa kifo, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki msingi za binadamu.

Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai. Serikali pia inapaswa kuheshimu haki ya wazazi kuwalea na kuwafunda watoto wao bila ya kuwatumbukiza katika mambo ambayo ni kinyume cha maadili na utu wema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linawaalika waamini na wananchi wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali na kuwaombea  mashuhuda wa Imani ya Kikristo wanaoendelea kumwaga damu yao sehemu mbali mbali za dunia; ni watu wanaohubiri Injili ya kwa njia ya maisha. Tarehe 25 Machi 2015, kuna fanyika maandamano ya kutetea Injili ya Uhai nchini Peru kama zilivyo sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.