2015-03-24 09:39:00

Shikamaneni katika upendo, ili kuwatangazia watu Injili ya Matumaini!


Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo kama alivyofanya Bikira Maria alipomtembelea binamu yake Elizabeth aliyekuwa mjamzito. Ni Mama ambaye alibahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, kiasi cha kushiriki kikamilifu katika mpango na historia ya ukombozi. Ni Mama mnyenyekevu na mwanafunzi makini wa Yesu aliyejifunza na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake mtakatifu, kiasi hata cha kusimama chini ya Msalaba.

Ni Mama anayefahamu mapungufu ya binadamu, madonda na magonjwa yanayo mwandama mwanadamu katika maisha yake ya kila siku.  Anafahamu mahangaiko ya vijana, familia na wazee kwa nyakati hizi, changamoto kwa Wafuasi wa Kristo kuendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe; kwa njia ya mshikamano wa upendo pamoja na kuwatangazia watu Injili ya Furaha na Matumaini.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mia tatu tangu kuanzishwa kwa Madhabahu ya Bikira Maria kitaifa ya Mariapocs yaliyofanyika, Jumatatu tarehe 23 Machi 2015, kwenye Kanisa kuu la Hajdudorog, nchini Hungaria. Amewashukuru waamini ambao kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wamesaidia kuendeleza Uinjilishaji hata katika mazingira magumu na hatarishi.

Kanisa daima linaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, uhuru wa kuabudu na mafao ya wengi. Ni wajibu kwa wananchi kujifunza kutambua kwamba, wao hata katika tofauti zao ni Familia ya Mungu. Kanisa ni Mama kwani ana dhamana ya kuhakikisha kwamba, anaendelea kuwarithisha watu zawadi ya maisha, imani na matumaini; ni mwalimu wa maadili na utu wema na mhudumu wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anatumwa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Leonardo Sandri anaitakia kheri na baraka Familia ya Mungu nchini Hungaria wakati huu inapoadhimisha na kukumbuka matendo makuu ya Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.