2015-03-24 10:16:00

Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu ni hija ya toba na wongofu wa ndani


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, madhulumu ya Wakristo huko Mashariki ya Kati; imani na matumaini kwa Rais Sergio Mattarella katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na majanga ambayo wahamiaji na wakimbizi wanaendelea kukabiliana nayo kwenye tumbo la Mediterrania, ni kati ya mambo yaliyozungumzwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumatatu, tarehe 23 Machi 2015.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa Familia ya Mungu nchini Italia kujikita katika Injili ya Kristo kwa kujitahidi kuwa ni watu wenye huruma kama Mwenyezi Mungu alivyo na huruma kwa waja wake. Yesu Kristo ni kielelezo makini cha huruma ya Mungu na kwamba, maadhimisho haya ni zawadi kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa la Kristo. Ni changamoto ya kufanya toba na wongofu wa ndani katika maisha ya mtu binafsi na Kanisa katika ujumla wake.

Huu ni mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Huruma ya Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo ambaye ameonesha mshikamano wa dhati na binadamu katika Fumbo la Umwilisho, mateso na kifo na chake. Yesu ndiye Msamaria mwema, anayejishusha chini ili kuwaganga wale waliopondeka moyo kwa mafuta ya huruma ya Mungu na divai ya Sakramenti za Kanisa. Kardinali Bangasco anawaalika waamini kuendelea kushikamana na Watawa wanapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, kwa kutambua na kuthamini mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia.

Kardinali Bagnasco anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na nyanyaso, dhuluma na mauaji ya Wakristo huko Mashariki ya Kati kutokana na chuki za kiimani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua kwamba, Injili ya Kristo imesaidia kwa kiasi kikubwa kujenga na kuimarisha: usawa, demokrasia ya kweli, utu na heshima ya binadamu.

Maaskofu wanalaani mauaji yote ya kinyama yanayoendelea kufanywa dhidi ya Wakristo na kwamba, wataendelea kushikamana nao kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo na udugu katika kipindi hiki kigumu cha historia ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu, heshima na utamaduni wa watu mahalia unaoanza kufutika kutokana na chuki za kidini.

Maaskofu wanapenda kuonesha moyo wa ushirikiano na mshikamano katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kana kwamba, ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Italia. Hapa kuna haja ya kubadili mwelekeo kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Hii ni kashafa dhidi ya watu wema, wakweli na waamini; ni dhambi dhidi ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wahamiaji pamoja na wakimbizi wanaohatarisha maisha yao kwa kutafuta nafuu ya maisha hata wakati mwingine kwa kuhatarisha maisha yao Jangwani na kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania ambako kuna watu wanaoendelea kupoteza maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.